Saturday, February 8, 2014

YANGA YAIFUNGA TIMU YA KOMOROZINE BAO 7 - 0

Ubao wa Matokeo.
 Mshambuliaji wa Timu ya Yanga,Hamis Kiiza akiipachikia timu yake bao la nne kati ya saba yaliyotiwa kimiani,wakati wa mchezo wao wa Klabu Bingwa Barani Afrika uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Yanga inaongoza kwa Bao 7-0.
 Mshambuliaji wa Yanga,Mrisho Ngassa akiondoka na mpira huku mabeki wa timu ya Komorozine ya nchini Comoro wakimsindikiza wakati wa mchezo wao wa Klabu Bingwa Barani Afrika uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Yanga inaongoza kwa Bao 7-0.
 Mrisho Ngassa bado yuko na mpiraaaaa.....
 Mrisho Ngassa anapachika bao paleeeee...... Gooooooooo ni goli la sita hili linaungwa hivi sasa na Mrisho Ngassa na kuwa mchezaji pekee aliefunga bao tatu peke yake.
Wachezaji wa timu ya Komorozine wakilaumiana.
 Mshambuliaji wa Pembeni wa Timu ya Yanga,Simon Msuva (27) akiwatoka mabeki wa timu ya Komorozine ya nchini Comoro wakati wa mchezo wao wa Klabu Bingwa Barani Afrika uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Yanga inaongoza kwa Bao 7-0.
 Mshambuliaji wa Pembeni wa Timu ya Yanga,Simon Msuva (27) akichuana vikali na Beki wa Timu ya Komorozine ya nchini Comoro,Ahmad Houmadi (5) wakati wa mchezo wao wa Klabu Bingwa Barani Afrika uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Yanga inaongoza kwa Bao 7-0.
 Wachezajiwa timu ya Yanga wakishangilia bao lao la pili lililotiwa kimiani na Mchezaji Nadir Haroub.
 Kiungo Mshambuliaji wa Yanga,Haroun Niyonzima akiafanya makeke yake wakati alipotaka kumtoka Beki wa Timu ya Komorozine ya nchini Comoro,Ali Mohamed wakati wa mchezo wao wa Klabu Bingwa Barani Afrika uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Yanga inaongoza kwa Bao 7-0.
 Mashabikiwa Timu ya Yanga.Picha zote na Othman Michuzi.

Friday, February 7, 2014

RAIS WA TFF JAMAL MALINZI AZUNGUMZIA MAFANIKIO YA UONGOZI WAKE NDANI YA SIKU 100

 Rais wa shirikisho la Mpira wa miguu nchini TFF Ndugu Jamal Malinzi katikati akizungungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo juu ya mafanikio ya uongozi wake kwa siku mia moja toka waingie madarakani, Kulia ni Afisa habari wa TFF Bonifas Wambura na kushoto ni Mshauri wa ufundi Bwana Rutayunga Peregenus
 Pichani ni baadhi ya Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakifuatilia mkutano huo uliofanyika leo ndani ya moja ya ukumbi wa hotel ya Kempisk Hyatt Regency Hotel,jijini Dar.

Friday, January 17, 2014

RAIS WA TFF AKITEUA KITUO CHA ALLIANCE ACADEMY KUWA KITOVU CHA MAANDALIZI YA U17 WA MWAKA 2019

ZIARA ya Rais wa TFF Jamal malinzi hatimaye imemelizika leo hapa jijini Mwanza kwa matukio mawili makubwa kufanyika.

Tukio la Kwanza limefanyika majira ya saa 2:30 katika ofisi za Halmashauri ya jiji la Mwanza ambapo Shirikisho hilo limesaini mkataba kati yake na Halmashauri hiyo kwaajili ya kuboresha uwanja wa Nyamagana.

Ili ipate kumwaga fedha zake za msaada kiasi cha dola laki 5 ambapo nyingine dola laki 1 zitatoka Halmashauri ya jiji la Mwanza, FIFA  ilikuwa ikitaka uthibitisho toka TFF kuwa uwanja huo kwa miaka yote utatumika kwa matumizi ya michezo yaani soka na si vinginevyo  kwaajili ya kuanza uboreshaji wa uwanja huo uliokuwa na utata wa kutaka kubadilishwa matumizi.

Tukio la pili Malinzi na timu yake ya wataalamu toka TFF, majira ya saa 4 asubuhi imetembelea na kukikagua kituo cha elimu na soka cha Alliance Academy ikiwa ni mwanzo wa mpango wa kitaifa wa kuwekeza katika soka la vijana.
Jamal Malinzi alipata fursa ya kuzungumza na wachezaji na wanafunzi vijana wanaochukua masomo ya usimamizi na uamuzi wa michezo (marefa), kikubwa sanjari na kuzingatia michezo pia alisisitiza kuiweka elimu mbele. 
Tofauti na eneo la kukaa watazamaji kwa kila kiwanja, katika eneo hili vimeunganika viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita 100 kila kimoja (nazungumzia maeneo ya kuchezea) na kingine kilichopo eneo la mabweni ya wasichana, ambapo TFF kupitia rais wake Jamal Malinzi imeahidi kuvikarabati viwanja hivi kwa kuvisawazisha kwa greda, kuviwekea magoli ya kisasa, kuweka udongo wenye rutuba na kuviwekea nyasi za kupanda zenye kiwango.

Tuesday, January 14, 2014

TAIFA STARS KUIKABILI NAMIBIA FIFA DATE

TAIFA STARS KUIKABILI NAMIBIA FIFA DATE
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia (Brave Warriors) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika (AFCON) zitakazochezwa mwakani nchini Morocco.

Stars na Brave Warriors zitacheza mechi hiyo Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia. Mechi hiyo ipo katika kalenda ya mechi za kirafiki za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Makubaliano ya kucheza mechi hiyo yamefikiwa kutokana na mazungumzo kati ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Namibia (NFA), John Muinjo.

Benchi la Ufundi la Brave Warriors linaongozwa na kocha mzawa Ricardo Mannetti, na mechi hiyo itachezwa ama Uwanja wa Sam Nujoma au Uwanja wa Uhuru jijini Windhoek.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inafundishwa na kocha Kim Poulsen kutoka Denmark na inatarajia kuanza kucheza mechi za mchujo za AFCON Septemba mwaka huu.
  
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Sunday, January 12, 2014

MALINZI AZINDUA KAMPENI YA ISHI HURU

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akizungumza wakati wa kuzindua programu ya kutoa elimu ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana iitwayo Ishi Huru.

Sunday, December 29, 2013

Chelsea vs Liverpool watched at Chalinze


Wednesday, December 25, 2013

Selestin Mwesigwa Katibu Mkuu mpya wa Shirikisho hilo la soka nchini

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akimtangaza Katibu Mkuu mpya wa Shirikisho hilo,ambaye ni Selestin Mwesigwa (aliewahi kuwa katibu mkuu wa Yanga) (wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria ya TFF,Wakili Evodius Mtawala (kulia) wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.Kushoto ni Afisa Habari wa TFF,Boniface Wambura.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (katikati) akimkabidhi Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria,Wakili Evodius Mtawala nakala ya ilani yake ya uchaguzi wakati akimtambulisha kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.kushoto ni Katibu Mkuu wa Mpya wa TFF,Selestin Mwesigwa.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (kulia) akimkabidhi Katibu Mkuu wa TFF, Selestin Mwesigwa nakala ya ilani yake ya uchaguzi wakati akimtambulisha kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

SHIRIKISHO la soka Tanzania,  TFF limemuajiri Katibu Mkuu wa zamani wa  Timu ya Yanga, Selestin Mwesigwa kuwa katibu mkuu mpya wa shirikisho hilo.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi imesema kuwa, Mwesigwa alizaliwa mwaka 1970,  ana digrii ya masuala ya kimataifa kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam na  diploma ya mafunzo ya sheria.

Malinzi aliongeza kuwa Mwesigwa amefanya kozi kadhaa za masuala ya utawala ndani na nje ya nchi zikiwemo kozi za utawala wa mpira zilizotolewa na FIFA.

 Rais huyo alisema Ajira yake ya  mwisho  ya Mwesigwa ilikuwa Ukatibu mkuu wa klabu ya Yanga ya Dar es salaam, hivyo ana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi ikizingatiwa amefanya kazi katika mashirika mbalimbali ikiwemo Plan International.

Aidha, Malinzi alisisitiza kuwa Mwesigwa alipokuwa katibu mkuu wa Yanga alishiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha Bodi ya Ligi kuu na ule wa Yanga kuingia udhamini na kampuni ya bia ya TBL, hivyo amekidhi vigezo vya kushika wadhifa huo mkubwa ndani ya TFF.

TFF pia imemuajiri katibu wa Simba SC, Wakili Evodius Mtawala kuwa Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria ya TFF.
Rais Malinzi alisema Mtawala  ana Shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  na Shahada ya Uzamili ya uongozi wa Biashara ya Chuo Kikuu cha ESAMI.

Rais aliongeza kuwa  Mtawala ambaye ajira yake ya mwisho ilikuwa Ukatibu mkuu wa Simba Sc , Klabu mwanachama wa TFF, ana uzoefu ambao utasaidia sana kukabili changamoto mbalimbali za vyama wanachama wa TFF.

Aidha Rais alisema uzoefu wake na ujuzi wa masuala ya sheria utasaidia kutatua masuala mbalimbali ya kisheria na kikatiba ndani ya shirikisho hilo.

Nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF imeachwa wazi kufuatia waombaji wote walioomba wa ndani na nje ya nchi kutokidhi vigezo, hivyo kamati ya utendaji imeagiza nafasi hii itangazwe upya na wale walioomba mara ya kwanza wasiombe tena.
Rais Malinzi alisema Bwana Idd Mshangama  atakaimu nafasi hii kwa sasa mpaka mtu mwingine atakapopatikana.

Pia nafasi ya Mkurugenzi wa ufundi imebaki wazi baada ya waombaji wote kutokidhi vigezo, hivyo Bwana Salum Madadi atakaimu nafasi hiyo na Rais Malinzi ameagiza itangazwe tena na walioomba wasiombe tena.

Nafasi nyingine iliyobaki wazi ni Mkurugenzi wa fedha na utawala, hivyo itatangazwa tena na kwasasa Bwana Danny Msangi atakaimu.
Afisa habari wa TFF ataendelea kuwa Bwana Boniface Wambura Mgoyo.

Rais Malinzi alisema ajira zote zitaanza rasmi januari Mosi mwakani na anawatakia kazi njema, huku akiwa na imani kubwa kuwa watasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira wa miguu.

Katika hatua nyingine, TFF imeteua wajumbe wa kamati ya uchaguzi na kamati ya Rufani ya Uchaguzi na kamati ya soka la ufukweni.
Kamati ya uchaguzi inaundwa  na Mwenyekiti, Wakili Melchesedek Lutema, Makamu wake, Wakili Walter Chipeta na Wajumbe Hamidu Mahmoud Omar, Jeremiah John Wambura na Hassan Dalali.

Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF itakuwa chini ya Mwenyekiti , Wakili Julius Lugaziya, Makamu wake,  Wakili Mwita Mwaisaka na Wajumbe Juma Abeid Khamis, Rashid Dilunga na Masoud Issangu.

Na kamati ya Soka la Ufukweni itakuwa chini ya Mwenyekiti Ahmed Mgoyi, makamu mwenyekiti, Shafii Dauda  na Wajumbe Deo Lucas, Juma Mgunda, Boniphace Pawasa, Joseph Kanakamfumu na John Mwansasu.

Monday, December 23, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu TFF

MECHI YA MTANI JEMBE YAINGIZA MIL 422/-
Mechi ya Nani Mtani Jembe kati ya Yanga na Simba iliyochezwa juzi (Desemba 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza sh. 422,611,000.

Mapato hayo ni kutokana na washabiki 52,589 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 40,000. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo walikuwa 19,044.

Asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa kutokana na mapato hayo ni sh. 64,466,084.75 wakati gharama za kuchapa tiketi ni sh. 7,488,000.

Mgawo mwingine ilikuwa kama ifuatavyo; kila klabu imepata sh. 117,470,066.61, asilimia 15 ya uwanja ni sh. 52,598,537.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 35,065,691.53 wakati gharama za mchezo zilikuwa sh. 28,052,553.22.

MALINZI, MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Desemba 24 mwaka huu).

Mkutano huo utafanyika saa 6 kamili mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

 Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Monday, December 16, 2013

Airtel yapiga tafu timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17

 Mchezaji wa zamani wa klabu ya Manchester United Andy Cole (kushoto) akiwasalimia vijana chini ya miaka 17 kabla ya kukutana na timu ya vijana wa timu ya Taifa chini ya miaka 17 katika viwanja vya Karume jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Slaa. 
 Mchezaji wa zamani wa klabu ya Manchester United Andy Cole (kushoto) akiwasalimia vijana chini ya miaka 17 kabla ya kukutana na timu ya vijana wa timu ya Taifa chini ya miaka 17 katika viwanja vya Karume jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Slaa.  
 Mchezaji wa zamanai wa Manchester United Andy cole(wa pili kulia) akisisitiza jambo kabla ya kujumuika na vijana wa timu ya Taifa chini ya miaka 17 jana - Dar es Salaam. Wengine ni Mkurugenzi mtendaji wa Airtel Tanzania Bwana Sunil Colaso na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. 
 Meya wa manispaa ya Ilala(wa pili kushoto) akikabidhi mipira iliyotolewa na Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Bwana Jamali Malinzi (kushoto) katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni mchezaji wa zamani wa klabu Manchester UnitedAndy Cole na Mkurugenzi mtendaji wa Airtel Sunil Colaso(kulia). 

Friday, December 6, 2013

mkutano wa makocha waandamizi kujadili mustakabali wa Taifa Stars waanza leo visiwani Zanzibar

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe ambaye bia yake inadhamini Taifa Stars, akitoa mada wakati wa ufunguzi wa mkutano unaojumuisha wataalamu mbalimbali kutoka Tanzania bara na Zanzibar ili kuangalia namna ya kuboresha Timu ya Taifa (Taifa Stars). Waliokaa kutoka kushoto ni Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina, Rais wa TFF Jamal Malinzi, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar, Hamisi Said na Makamu wa Rais wa ZFA Ali Mohamed Ali. Mkutano huo wa siku tatu unaodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager unafanyika katika hoteli ya Mtoni Marine visiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar, Hamisi Said (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na jopo la makocha na wakufunzi maarufu nchini wanaokutana Visiwani Zanzibar kuangalia namna ya kuboresha Timu ya Taifa Taifa Stars. Wengine waliokaa kutoka kushoto ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager George Kavishe, Makamu wa Rais wa ZFA Ali Mohamed Ali, Rais wa TFF Jamal Malinzi, Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina, mwenyekiti wa jopo hilo la wataalamu, Kanali mstaafu Idd Kipingu na Katibu wake Rutayuoga Pelegrinius.

Wednesday, December 4, 2013

RAIS WA TFF AUNDA JOPO LA WATAALAMU 20 KUPANGA MKAKATI WA KUCHEZA AFCON 2015

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es salaam leo wakati wa kutangaza Jopo la wataalamu 20 aliowateua kwa ajili ya kupanga mkakati wa kutengeneza timu itakayoweza kuonyesha jinsi Tanzania inavyoweza kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2015 nchini Morocco. Jopo hilo la wataalam litakutana kwa siku tatu mjini Zanzibar kuanzia Desemba 6-8 mwaka huu. Jopo hilo litaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Omari Kipingu.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Lager,George Kavishe akizungumza machache juu ya Kamati hiyo maalum,ambapo ameiombea mafanikio makubwa ili tuweze kuja kupata timu bora ya Taifa kwa siku zijazo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Jopo la wataalamu 20 watakaokutana Visiwani Zanzibar hivi karibuni,Kanali mstaafu Idd Omari Kipingu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam leo.
Mmoja wa Waandishi wa habari kutoka Chombo cha EATV,Patrick Nyembela akiuliza swali kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (hayupo pichani). 

Jopo la wataalamu 20 walioteuliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi linakutana kupanga mkakati wa kuonesha jinsi Tanzania inavyoweza kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2015 nchini Morocco.

Kikao hicho maalumu (retreat) kitafanyika mjini Zanzibar kuanzia Desemba 6-8 mwaka huu. Jopo hilo litaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Omari Kipingu.

Wengine wanaounda jopo hilo linalohusisha pia makocha ni Dk. Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub Nyenzi, Abdallah Kibaden, Pelegrinius Rutahyuga, Kidao Wilfred, Salum Madadi, Juma Mwambusi, Ken Mwaisabula, Boniface Mkwasa, Fred Minziro, Meja Abdul Mingange, Ally Mayay, Boniface Mkwasa na Dan Korosso.


Wajumbe wengine wa jopo hilo wanatoka Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).

Saturday, November 30, 2013

KAMATI ZA MAADILI ZAWATAKA WANACHAMA WA TFF KUBADILI KATIBA ZAO

Wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wanatakiwa kufanyia marekebisho katika katiba zao kwa kuingiza ibara ya Kamati za Maadili.

Maagizo hayo yanatokana na kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF iliyoketi Novemba 23 mwaka huu jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jamal Malinzi ambapo pamoja na mambo mengine ilijadili umuhimu wa wanachama wake kuunda kamati hizo.

Wanachama wa TFF ambao muda wao wa uchaguzi umekaribia, wanatakiwa kufanya marekebisho hayo kwanza kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi.

TFF ina aina tatu za wanachama. Wanachama hao ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na Klabu za ligi Kuu.

FAINALI YA KOMBE LA UHAI CHAMAZI
Mechi ya Fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu itachezwa keshokutwa (Jumapili) kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Coastal Union ndiyo itakayocheza fainali hiyo kuanzia saa 9.30 alasiri dhidi ya mshindi wa mechi ya nusu fainali ya pili kati ya Yanga na Mtibwa Sugar inayotarajia kuchezwa baadaye leo.

Mechi ya fainali itatanguliwa na ile ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Azam na timu itakayoshindwa katika mechi ya pili ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu iliyoanza katika viwanja vya Karume na DUCE kabla ya kuhamia Chamazi.

Wednesday, November 20, 2013

Airtel yazindua promosheni ya MIMI NI BINGWA ikishirikiana na klabu ya Manchester United

 Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, Bw. Sunil Colaso akimkabidhi jezi ya Timu ya Manchester United, raisi mpya wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania Bw. Jamal Malinzi
 Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, Sunil Colaso akimkabidhi jezi ya Timu ya Manchester United mtangazaji wa Clouds FM, Bw. Ephraim Kibonde ambaye alichukua kwa niaba ya wapenzi wa mpira.
Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, Bw. Sunil Colaso (wa pili kutoka kushoto) akiwa pamoja na Meneja Uhusiano wa Timu ya Manchester United, Bw. Michael Higham  (wa kwanza kushoto). Kutoka kulia niMkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Bw.  Leornad Thadeo, Raismpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Mtangazaji wa Clouds FM, Bw. Ephraim Kibonde muda mfupi baada ya uzinduzi wa promosheni ya ‘MIMI NI BINGWA’ iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam. 

Saturday, November 16, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


MALINZI KUFUNGUA MICHUANO YA UHAI 2013

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi  (pichani) atafungua rasmi michuano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 (U20) kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom mwaka huu.

Uzinduzi wa mashindano hayo utafanyika kesho (Novemba 17 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam saa 2 kamili asubuhi. Mechi ya ufunguzi itakuwa ya kundi A kati ya Azam na Coastal Union.

Mechi nyingine za kesho ni kundi; Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Uwanja wa Karume), kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United (saa 4 asubuhi- Uwanja wa Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Uwanja wa Karume).

Kundi C kutakuwa na mechi kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itakayochezwa saa 2 kamili asubuhi kwenye Uwanja wa Azam Complex, na kwenye uwanja huo huo saa 10 jioni ni Rhino Rangers dhidi ya Tanzania Prisons.
RAMBIRAMBI MSIBA WA NYOTA COPA COCA-COLA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Sayari, Fatuma Bahau ‘Crouch’ kilichotokea jana (Novemba 15 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika mpira wa miguu kwani Fatuma ndiyo kwanza alikuwa anachipukia katika mpira wa miguu wa wanawake ambapo alikuwa mfungaji bora wa michuano ya U15 Copa Coca-Cola ya mwaka huu akichezea timu ya Ilala, hivyo mchango wake katika mchezo huu tutaukumbuka daima.

Kwa mujibu wa mlezi wa mchezaji huyo, Stephania Kabumba, marehemu anasafirishwa kesho kwenda kwao Mwanza kwa ajili ya maziko ambapo kifo chake kimesababishwa na ugonjwa wa malaria.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bahau, klabu ya Sayari, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Fatuma mahali pema peponi. Amina

 Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Sunday, November 3, 2013

JAMAL MALINZI AMTEUA BONIFACE WAMBURA KUWA KAIMU KATIBU MKUU TFF

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Bw. Boniface Wambura (kulia) kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF. Uteuzi huo ni kuanzia Novemba 2 mwaka huu.

Aidha aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah (kushoto) ameagizwa aende likizo ya malipo hadi atakapomaliza mkataba wake.
 Kamati ya Utendaji inaviomba vilabu, vyama vya wilaya, vyama vya mikoa, vyama shiriki na wadau wote kumpa ushirikiano Bw. Boniface Wambura katika utekelezaji wa majukumu yake.
  
Jamal Malinzi
Rais TFF 


Dar es Salaam 
Novemba 3, 2013

Thursday, October 31, 2013

TAARIFA ZA MICHEZO KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

SALAMU ZA PONGEZI ZAMIMINIKA KWA MALINZI.


Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Jamal Malinzi ameendelea kupokea salamu za pongezi baada ya kushinda wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.



Salamu nyingine za zimetoka kwa Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter ambapo amempongeza Malinzi kwa kuchaguliwa na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake ya kuongoza mchezo huo nchini.



Blatter amesema ana uhakika ufahamu wake na uwezo wake katika uongozi ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini, na kuongeza kuwa milango ya FIFA iko wazi wakati wowote anapotaka kujadili masuala yanayohusu mchezo huo.



“Nakutakia wewe na kamati mpya ya Utendaji iliyochaguliwa kila la kheri, nguvu, na kila aina ya mafanikio kwa changamoto zilizo mbele yenu,” amesema Rais Blatter katika salamu zake.



Wengine waliomtumia Rais Malinzi salamu za pongezi ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya, Rais wa Heshima wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Arumeru (ADFA), Peter Temu.



YANGA, JKT RUVU UWANJANI KESHO

Raundi ya 12 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Novemba 1 mwaka huu) kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Yanga itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.



Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A. Tiketi zitauzwa siku ya mechi uwanjani katika magari maalumu kuanzia saa 4 asubuhi.




Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).



Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.



Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.



Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.



Boniface Wambura Mgoyo

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Wednesday, October 30, 2013

RAIS WA CAF AMPONGEZA RAIS JAMAL MALINZI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.



Katika salamu zake kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya mpira wa miguu Afrika, Rais Hayatou amesema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi fursa ya kuupeleka mbele mpira wa miguu nchini Tanzania.



Amesema CAF ina imani uwezo wake katika uongozi, uzoefu na ujuzi katika mpira wa miguu havitausaidia mpira wa miguu Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla, na kuongeza kuwa ataendeleza ushirikiano uliopo ili kuwanufaisha zaidi vijana wa bara hili.



Rais Hayatou amemtakia Rais Malinzi kila la kheri katika kipindi chake cha uongozi na kumhakikishia kuwa CAF iko pamoja naye katika kusukuma mbele gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu.



PAMBANO LA YANGA, MGAMBO SHOOTING LAINGIZA MIL 37/-

Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Mgambo Shooting lililochezwa jana (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 37,915,000.



Washabiki waliohudhuria mechi hiyo namba 46 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 walikuwa 6,515 ambapo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.



Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 5,783,644.07, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,145,790 wakati kila klabu ilipata sh. 8,550,741.95.



Wamiliki wa uwanja walipata sh. 4,347,834.89, gharama za mchezo sh. 2,608,700.93, Bodi ya Ligi sh. 2,608,700.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,304,350.47, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,014,494.81.



SIMBA, KAGERA SUGAR KUUMANA KESHO

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaanza raundi ya 12 kesho (Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.



Viingilio katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kupitia TBC 1 vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.



Nayo Yanga itashuka uwanjani Novemba Mosi mwaka huu katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.



Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).



Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.



Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.



Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.



Boniface Wambura Mgoyo

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation