Wednesday, December 25, 2013

Selestin Mwesigwa Katibu Mkuu mpya wa Shirikisho hilo la soka nchini

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akimtangaza Katibu Mkuu mpya wa Shirikisho hilo,ambaye ni Selestin Mwesigwa (aliewahi kuwa katibu mkuu wa Yanga) (wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria ya TFF,Wakili Evodius Mtawala (kulia) wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.Kushoto ni Afisa Habari wa TFF,Boniface Wambura.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (katikati) akimkabidhi Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria,Wakili Evodius Mtawala nakala ya ilani yake ya uchaguzi wakati akimtambulisha kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.kushoto ni Katibu Mkuu wa Mpya wa TFF,Selestin Mwesigwa.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (kulia) akimkabidhi Katibu Mkuu wa TFF, Selestin Mwesigwa nakala ya ilani yake ya uchaguzi wakati akimtambulisha kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

SHIRIKISHO la soka Tanzania,  TFF limemuajiri Katibu Mkuu wa zamani wa  Timu ya Yanga, Selestin Mwesigwa kuwa katibu mkuu mpya wa shirikisho hilo.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi imesema kuwa, Mwesigwa alizaliwa mwaka 1970,  ana digrii ya masuala ya kimataifa kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam na  diploma ya mafunzo ya sheria.

Malinzi aliongeza kuwa Mwesigwa amefanya kozi kadhaa za masuala ya utawala ndani na nje ya nchi zikiwemo kozi za utawala wa mpira zilizotolewa na FIFA.

 Rais huyo alisema Ajira yake ya  mwisho  ya Mwesigwa ilikuwa Ukatibu mkuu wa klabu ya Yanga ya Dar es salaam, hivyo ana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi ikizingatiwa amefanya kazi katika mashirika mbalimbali ikiwemo Plan International.

Aidha, Malinzi alisisitiza kuwa Mwesigwa alipokuwa katibu mkuu wa Yanga alishiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha Bodi ya Ligi kuu na ule wa Yanga kuingia udhamini na kampuni ya bia ya TBL, hivyo amekidhi vigezo vya kushika wadhifa huo mkubwa ndani ya TFF.

TFF pia imemuajiri katibu wa Simba SC, Wakili Evodius Mtawala kuwa Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria ya TFF.
Rais Malinzi alisema Mtawala  ana Shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  na Shahada ya Uzamili ya uongozi wa Biashara ya Chuo Kikuu cha ESAMI.

Rais aliongeza kuwa  Mtawala ambaye ajira yake ya mwisho ilikuwa Ukatibu mkuu wa Simba Sc , Klabu mwanachama wa TFF, ana uzoefu ambao utasaidia sana kukabili changamoto mbalimbali za vyama wanachama wa TFF.

Aidha Rais alisema uzoefu wake na ujuzi wa masuala ya sheria utasaidia kutatua masuala mbalimbali ya kisheria na kikatiba ndani ya shirikisho hilo.

Nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF imeachwa wazi kufuatia waombaji wote walioomba wa ndani na nje ya nchi kutokidhi vigezo, hivyo kamati ya utendaji imeagiza nafasi hii itangazwe upya na wale walioomba mara ya kwanza wasiombe tena.
Rais Malinzi alisema Bwana Idd Mshangama  atakaimu nafasi hii kwa sasa mpaka mtu mwingine atakapopatikana.

Pia nafasi ya Mkurugenzi wa ufundi imebaki wazi baada ya waombaji wote kutokidhi vigezo, hivyo Bwana Salum Madadi atakaimu nafasi hiyo na Rais Malinzi ameagiza itangazwe tena na walioomba wasiombe tena.

Nafasi nyingine iliyobaki wazi ni Mkurugenzi wa fedha na utawala, hivyo itatangazwa tena na kwasasa Bwana Danny Msangi atakaimu.
Afisa habari wa TFF ataendelea kuwa Bwana Boniface Wambura Mgoyo.

Rais Malinzi alisema ajira zote zitaanza rasmi januari Mosi mwakani na anawatakia kazi njema, huku akiwa na imani kubwa kuwa watasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira wa miguu.

Katika hatua nyingine, TFF imeteua wajumbe wa kamati ya uchaguzi na kamati ya Rufani ya Uchaguzi na kamati ya soka la ufukweni.
Kamati ya uchaguzi inaundwa  na Mwenyekiti, Wakili Melchesedek Lutema, Makamu wake, Wakili Walter Chipeta na Wajumbe Hamidu Mahmoud Omar, Jeremiah John Wambura na Hassan Dalali.

Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF itakuwa chini ya Mwenyekiti , Wakili Julius Lugaziya, Makamu wake,  Wakili Mwita Mwaisaka na Wajumbe Juma Abeid Khamis, Rashid Dilunga na Masoud Issangu.

Na kamati ya Soka la Ufukweni itakuwa chini ya Mwenyekiti Ahmed Mgoyi, makamu mwenyekiti, Shafii Dauda  na Wajumbe Deo Lucas, Juma Mgunda, Boniphace Pawasa, Joseph Kanakamfumu na John Mwansasu.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation