Friday, April 29, 2011

USAJILI KILI TAIFA CUP 2011

Timu zote 24 zilizothibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Taifa mwaka huu
(Kili Taifa Cup 2011) zimewasilisha usajili wa wachezaji wao ndani ya muda
uliopangwa. Timu hizo na vituo vyao kwenye mabano ni Mtwara, Ruvuma, Kinondoni
na Lindi (Lindi).
Nyingine ni Mbeya, Iringa, Temeke na Rukwa (Mbeya), Dodoma, Tabora, Singida na
Kigoma (Tabora), Arusha, Kilimanjaro, Tanga na U23 (Moshi), Mwanza, Kagera, Mara
na Shinyanga (Mwanza) na Pwani, Morogoro, Ilala na Manyara (Morogoro).
Siku ya mwisho kuweka pingamizi kwa wachezaji ni Mei 2 wakati siku ya mwisho kwa
Kamati ya Mashindano kuthibitisha usajili ni Mei 3 mwaka huu. Timu zinatakiwa
kuwasili vituoni Mei 5 na mashindano yataanza Mei 7.
HAKI ZA TELEVISHENI KILI TAIFA CUP 2011
TFF ilitangaza tenda kwa vituo vya televisheni nchini kuonesha moja kwa moja
(live) mashindano ya Kili Taifa Cup. Vituo viwili vya televisheni vilijitokeza
kutaka haki ya kuonesha michuano hiyo.
Baadaye kituo kimoja kilijitoa kutokana na sababu za kiufundi wakati kingine
kilishindwa kufikia dau ambalo limewekwa na TFF ili kupata haki hizo. Dau la
kuonesha ‘live’ michuano hiyo ni sh. milioni 10. Hivyo hadi sasa hakuna
televisheni yenye haki ya kuonesha michuano hiyo.
Bado tunakaribisha vituo vyenye nia ya kuonesha mashindano hayo moja kwa moja
kwa mazungumzo. Hivyo tutatoa taarifa baadaye juu ya nini kinaendelea kabla ya
mashindano yenyewe kuanza, hasa hatua ya mtoano (knock out).
Boniface Wambura
Ofisa Habari

PRESS CONFERENCE YA U23

Makocha wa Tanzania U23, Jamhuri Kihwelo na Uganda U23 (The Kobs),
Bob Williams watakuwa na mkutano na waandishi wa habari.

Siku: Ijumaa
Tarehe: Aprili 29, 2011
Muda: Saa 5 kamili
Mahali: TFF

Regards

Boniface Wambura
TFF Media Officer

Tuesday, April 26, 2011

KIINGILIO MECHI YA U23 v UGANDA (THE KOBS) NI SH.1,000/-

Timu ya Taifa ya Tanzania (u23)
Timu ya Taifa ya Uganda (u23)

Mechi ya mchujo ya All Africa Games kati ya timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 (U23) na Uganda (The Kobs) itachezwa Aprili 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 1,000 kwa viti vya Kijani, Bluu na Rangi ya Chungwa (Orange straight and curve). Kwa upande wa VIP C na B itakuwa sh. 5,000 wakati sh. 10,000 ni kwa VIP A.

Tunatarajia kuanza kuuza tiketi siku moja kabla ya mchezo katika vituo vya Premier Betting (Kariakoo- Mtaa wa Sukuma, Buguruni Sokoni, Manzese Midizini, JM Mall na Tandale kwa Mtogole), Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Steers (Mtaa wa Ohio na Samora), Big Bon Msimbazi (Kariakoo) na Uwanja wa Uhuru.

Timu ya Taifa ya Uganda chini ya umri wa miaka 23 (The Kobs) inatarajia kuwasili nchini Alhamisi (Aprili 28 mwaka huu) saa 10.30 jioni kwa ndege ya Uganda Air na kurejea nyumbani Jumapili (Mei 1 mwaka huu) saa 11.50 kwa ndege hiyo hiyo.

Msafara wa timu hiyo utaongozwa na Ofisa wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) Sam Lwere na utafikia hoteli ya Durban iliyoko Barabara ya Uhuru, Dar es Salaam.

Timu ya U23 ya Tanzania iko kambini hoteli ya Bamba Beach iliyoko Kigamboni tangu iliporejea kutoka Uganda na inaendelea na mazoezi chini ya Kocha wake Mkuu, Jamhuri Kihwelo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Sunday, April 24, 2011

TAIFA STARS YAFUNGWA 2-0 DHIDI YA MSUMBIJI

MABAO mawili ya mshambuliaji Jeremias Sitoe katika kila kipindi yameipatia
Msumbiji (Mambas) ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika usiku (Aprili 23 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, jijini hapa.

Mechi hiyo maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa uwanja huo wa kisasa uliojengwa na Wachina na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji ilikuwa ya ushindani wa hali ya juu. Rais Armando Guebuza wa Msumbiji ndiye aliyezindua uwanja huo.

Sitoe alifunga mabao hayo dakika ya 19 na 51 karibu kwa staili ileile baada ya
mabeki wa kati Aggrey Morris na Nadir Haroub 'Cannavaro' kujichanganya katika kucheza mipira mirefu aliyopigiwa mshambuliaji huyo mwenye kasi na pia kudhani ameotea.

"Ni matokeo mabaya, lakini mmecheza mchezo mzuri na ari yenu ilikuwa juu huku mkijituma vizuri. Bado tunatakiwa kuongeza umakini katika kuwahi mipira," alisema Kocha Jan Poulsen akiwaambia wachezaji wake mara baada ya mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka Swaziland.

Stars iliyocheza vizuri zaidi kipindi cha pili huku kwa muda mwingi ikiwa eneo
la wapinzani wao, kulinganisha na kile cha kwanza ilifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Mambas. Washambuliaji John Boko, Salum Machaku na Mwinyi Kazimoto walipata nafasi za kufunga kipindi cha kwanza lakini ama waliwahiwa na mabeki au mipira yao iliokolewa na kipa Joao Kampango.

Poulsen alikianza kipindi cha pili kwa kuwatoa Shabani Dihile, Mohamed Banka, Kazimoto na Machaku, na nafasi zao kuchukuliwa na Juma Kaseja, Ramadhan Chombo 'Redondo', Mbwana Samata na Julius Mrope. Mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mchezo kwa upande wa Stars ambayo ilishuhudia nahodha wake Shadrack Nsajigwa na Cannavaro wakionywa kwa kadi za njano na mwamuzi Simanga Hhleko.

Mambas ambao watashiriki michezo ya All Africa Games itakayofanyika hapa
Septemba mwaka huu walicheza kwa pasi fupi fupi na kuongeza kasi kila walipokuwa wakikaribia lango la Taifa Stars.

Poulsen aliwataka wachezaji kutumia vizuri wiki moja iliyobaki kwa ajili ya
mapumziko, kwani atawaita tena kambini Mei 2 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya fainali za Kombe la mataifa ya Afrika zitakazochezwa mwakani Gabon- Equatorial Guinea dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mechi hiyo itachezwa jijini Bangui, Juni 4 mwaka huu.

Stars: Dihile/Kaseja, Nsajigwa, Amir Maftah, Morris, Cannavaro, Shabani Nditi,
Banka/Redondo, Nurdin Bakari, Boko, Kazimoto/Samata na Machaku/Mrope.

Mambas: Kampango, Momed Hagi, Eugenio Bila, Eduardo Jumisse/Stelio Ernesto,Carlos Chimomole/Arlindo Cumaio, Sitoe/Danilo Manhonga, Samuel
Chapanga/Francisco Muchanga, Francisco Massinga, Almiro Lobo, Celcisio Bonifacio na Zainadine Junior.

Timu inarejea leo saa 12.45 jioni kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.

Authored by
Boniface Wambura
Media Officer
Tanzania Football Federation (TFF)

Saturday, April 23, 2011

Taifa stars kucheza na Msumbiji leo huko Maputo

TAIFA STARS

Maputo, Msumbiji
Taifa Stars iliwasili jana salama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maputo saa
5.52 asubuhi (saa 6.52 kwa saa za nyumbani) kwa ndege ya Kenya Airways ikitokea Nairobi. Timu iko hapa kwa ajili ya mechi ya ufunguzi wa Uwanja wa Taifa. Uwanja huo mpya ambao capacity yake ni watazamaji 40,000 umejengwa na Wachina na uko nje kidogo ya Jiji la Maputo ambapo ni wastani wa saa moja kwa gari kutoka mjini.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa uwanja atakuwa Rais wa Msumbiji wakati Rais Jakaya Kikwete anawakilishwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi. Timu imefikia hoteli ya VIP Grand ambapo jana saa 12.30 kwa saa za hapa ilifanya mazoezi Uwanja wa Taifa kwa dakika 45.

Mechi itaanza saa 12.30 jioni kwa saa za hapa, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Swaziland. Mwamuzi ni Simanga Hhleko wakati wasaidizi wake ni Bhekisizwe Mkhabela na Lybnah Sibiya. Fourth official ambaye ni wa hapa Msumbiji ni Estevao Matsinhe.

Taifa Stars line up;
Shabani Dihile (1)
Shadrack Nsajigwa (14)- captain
Amir Maftah (3)
Aggrey Morris (6)
Nadir Haroub (13)
Nurdin Bakari (5)
Mohamed Banka (16)
Shabani Nditi (19)
John Boko (9)
Machaku Salum (11)
Mwinyi Kazimoto (22)

Substitutes:
Shabani Kado (18)
Kigi Makasi (7)
Julius Mrope (8)
Ramadhan Chombo (21)
Jabir Aziz (12)
Mbwana Samata (10)
Juma Nyoso (4)

Officials:
Jan Poulsen- Head Coach
Sylvester Marsh- Assistant Coach
Juma Pondamali- Goal keeping Coach
Leopold Tasso- Team Manager
Dr Mwanandi Mwankemwa- Team Physician
Alfred Chimela- Kit Manager

Timu itaondoka hapa kurejea nyumbani kesho April 24 saa 11.35 kwa Kenya Airways hadi Nairobi ambapo itakaa kwa muda ikisubiri kubadili ndege kwa ajili ya safari ya Dar es Salaam.

My contact in Maputo +258 767 310242
Boniface Wambura
Media Officer
Tanzania Football Federation


Tuesday, April 19, 2011

WAAMUZI SITA WA TANZANIA KUCHEZESHA ALL AFRICA GAMES

Waamuzi sita wa Tanzania wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mechi za raundi ya kwanza za All Africa Games zitakazochezwa Aprili 30 mwaka huu na Mei 14 mwaka huu. Waziri Sheha akisaidiwa na Hamis Chang’walu na John Kanyenye atachezesha mechi kati ya Malawi na Afrika Kusini itakayochezwa Aprili 30 mwaka huu nchini Malawi.

Judith Gamba akisaidiwa na Saada Hussein na Mwanahija Makame atachezesha mechi ya wanawake kwa michuano hiyo kati ya Zimbabwe na Angola. Mechi itafanyika Mei 14 mwaka huu nchini Zimbabwe. Naye Hafidh Ally ameteuliwa kuwa Kamishna wa mchezo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Gabon. DRC ndiyo wenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa Aprili 30 mwaka huu.

U23 v UGANDA
Mechi ya marudiano ya All Africa Games kati ya timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 dhidi ya Uganda itakayofanyika Aprili 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na Athanase Niyongabo kutoka Burundi.

Waamuzi wasaidizi ambao pia watatoka Burundi ni Jean-Marie Hakizimana na Felix Bazubwabo wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Ramadhan Ibada ‘Kibo’ wa Tanzania. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Gaspard Kaijuka kutoka Rwanda.

UCHAGUZI COASTAL UNION, VILLA SQUAD
Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake cha Aprili 13 mwaka huu iliarifiwa kuwa klabu ya Coastal Union ya Tanga inatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake hivi karibuni. Ili kufanikisha kikamilifu utekelezaji wa matakwa hayo ya Katiba, Kamati imeitaka Coastal Union kuandaa uchaguzi kwa kuzingatia Katiba ya Klabu inayoendana na Katiba ya mfano ya TFF kwa wanachama wake na pia kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF.

Pia Kamati ya Uchaguzi imefuta uchaguzi wa klabu ya Villa Squad ya Dar es Salaam kutokana na kutozingatia kwa utimilifu Kanuni za Uchaguzi. Mchakato wa uchaguzi utaanza tena mara baada ya Villa Squad kukamilisha taratibu za uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wananachama wa TFF.

NAFASI YA UKOCHA BOTSWANA
Klabu ya Gaborone United Sporting ya Botswana inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo kupitia TFF inasaka kocha mwenye sifa kwa ajili ya kufundisha kikosi chake kwa msimu ujao wa ligi.

Kwa mujibu wa tangazo la nafasi hiyo ya Kocha Mkuu lililotumwa TFF na Ofisa Uhusiano wa klabu hiyo Romeo Benjamin, moja ya sifa hizo ni kuwa na diploma ya ukocha ya chuo/taasisi inayotambulika. Mwisho wa kutuma maombi ni Aprili 30 mwaka huu.


Boniface Wambura
Ofisa Habari

Sunday, April 17, 2011

UGANDA 2 TANZANIA U23 1

Mechi: All Africa Games qualifying first leg (First round)
Uwanja: Mandela (Namboole) Kampala, Uganda
Matokeo: Uganda (The Kobs) 2 Tanzania U23- 1

Mabao ya Uganda yamefungwa na Moses Olaya (dk. 4) baada ya shuti lililopigwa na
mshambuliaji Owen kasule kumtoka kipa Shabani Kado. Kiiza Hamis alifunga la pili
(dk. 23) akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto.

Bao la Tanzania U23 limefungwa dakika ya 46 kwa shuti la mbali (katikati ya
uwanja) na Kigi Makasi.

Akizungumzia pambano hilo Kocha Jamhuri Kihwelo amesema ameyapokea matokeo,
hivyo atajipanga kwa mechi ya marudiano kwa kuufanyia kazi upungufu wote
uliojitokeza katika pambano hilo. Hata hivyo amekiri kuwa Uganda ni wazuri na
anatambua kuwa watajipanga vizuri zaidi kwa mechi ya marudiano.

U23: Shaaban Kado, Juma Abdul, Kigi Makasi, Babu Ally, Shomari Kapombe, Salum
Telela, Mrisho Ngasa, Jabir Aziz, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata na Khamis
Mcha/Awadh Juma.

The Kobs: Benjamin Ochan, Saka Mpiima, Godfrey Walusimbi, Ivan Bukenya, Isaac
Isinde, Kiiza Hamisi, Sadam Mussa, Moses Olaya/Siraje Turyamuhebwa, Owen Kasule,
Emmanuel Okwi/Moses Kaye na Mike Mutyaba/Brian Majwega.

U23 itarejea Dar es Salaam siku ya Jumatatu saa 8 mchana kwa ndege ya Air Uganda

Thursday, April 14, 2011

U23 KWENDA UGANDA LEO APRILI 14

Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 inatarajia kuagwa kesho
(Aprili 14 mwaka huu) saa 7 mchana katika ofisi za TFF kabla ya kuondoka saa
mbili baadaye kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya mchujo ya michezo ya Afrika (All Africa Games) itakayochezwa Jumamosi (Aprili 16 mwaka huu)

Msafara wa timu hiyo utakuwa na wachezaji 20 na benchi la ufundi lenye watu sita ukiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Hafidh Ally Tahir.

Wachezaji watakaokuwemo katika msafara huo niShaaban Kado, Juma Abdul, David Luhende, Babu Ally, Shomari Kapombe, Jabir Aziz, Salum Aboubakar, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata, Kigi Makasi, Gharib Mussa, Mbwana Bakari, Idrisa Abdulrahim, Innocent Wambura, Khamis Mcha, Awadh Issa, Amour Suleiman, Himid Mao, Mrisho Ngassa na Salum Telela.

Pia leo mchana (Aprili 13 mwaka huu) timu hiyo imekabidhiwa jumla ya sh. milioni 22 ambazo iliahidiwa endapo ingeitoa Cameroon kwenye michuano ya Olimpiki. Fedha hizo ziliahidiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kampuni ya Simba Trailers.

NSSF kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake Dk. Ramadhan Dau ilikabidhi sh. milioni 10 wakati Azim Dewji ambaye ni Mkurugenzi wa Simba Trailers alikabidhi sh. milioni 12. Kati ya fedha hizo ilizotoa Simba Trailers, sh. milioni 10 ni kwa ajili ya timu, sh. milioni mbili kwa ajili ya kipa aliyeokoa penalti na wafungaji wa mabao mawili ya U23.

U23 imepangiwa kucheza na Nigeria katika raundi ya pili ya michuano ya Olimpiki ambapo mechi ya kwanza itachezwa jijini Dar es Salaam kati ya Juni 4 na 5 mwaka huu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Wednesday, April 13, 2011

TBL pamoja TFF Wakutana na Wahariri wa Habari za Michezo kuzungumzia Kili Taifa Cup 2011

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro ambao ndio wadhamini wakuu wa Ligi ya Kili Taifa Cup 2011,George Kavishe akizungumza katika mkutano na Wahariri wa Habari za Michezo kutoka vyombo mbali mbali vya Habari juu ya mchakato mzima wa ligi ya Kili Taifa Cup 2011 utakavyokuwa,mkutano huu umefanyika mchana huu katika hoteli ya Paradise,Benjamin Mkapa jijini Dar.
Katibu Mkuu wa TFF,Angetile Osseah akijibu moja ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa na Wahariri wa Habari za Michezo katika mkutano uliofanyika mchana huu katika hoteli ya Paradise,Benjamin Mkapa tower,jijini Dar.
Meneja Habari na Mahusiano wa kampuni ya Excutive Solutions,Mike Mukunza akitoa muongozo kwa Wahariri wa Habari za Michezo wa vyombo mbali mbali vya Habari juu ya namna habari hizo zitakavyotakiwa kuwa katika vyombo hivyo.
Afisa wa Idara ya Ufundi (TFF),Saad Kawemba akijibu moja ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa na Wahariri wa Habari za Michezo.
Mkurugenzi wa Masoko wa TFF,Jimmy Kabwe,akizungumza katika mkutano huo.
Meza Kuu ikisikiliza maswali toka kwa wahariri wa Habari za Michezo.
Maulid Kitenge wa ITV/Radio One akiuliza swali kwa viongozi wa TFF.
Zubeiry Ismail wa Tanzania Daima akiuliza swali.
Mpangilio wa Mikoa katika Ligi ya Taifa.
Mkutano ukiendelea.

Tuesday, April 12, 2011

Tanzania v/s Cameroun U-23 highlights

H.E President Kagame of Rwanda

President Kagame of Rwanda H.E. Paul Kagame greets players accompanied by CECAFA secretary general Nicholaus Musonye during the Kagame Cup at the Amahoro Stadium in Kigali last year. This year the East and Central African Soccer clubs championships is sheduled to be held in Sudan after Zanzibar failed to host the regional tournament due to financial constraints

U23 KWENDA UGANDA APRILI 15


Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 inatarajia kuondoka nchini Aprili 15 mwaka huu kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya mchujo ya michezo ya Afrika (All Africa Games) itakayochezwa Jumamosi (Aprili 16 mwaka huu) Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Mandela (Namboole) kuanzia saa 10 kamili jioni itasimamiwa na Kamishna Jean-Didier Masamba Malunga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Waamuzi ni Nur Adbulle, Salah Abukar na Hassan Mohamed kutoka Somalia. U23 itakuwa na msafara wa watu 30 wakiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Hafidh Ally Tahir. Benchi la Ufundi litakuwa na watu sita wakiongozwa na Kocha Mkuu Jamhuri Kihwelo wakati wachezaji ni 20.

Timu inatarajia kurejea Dar es Salaam, Aprili 17 mwaka huu. Mechi ya marudiano itachezwa Aprili 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Michuano ya All Africa Games itafanyika jijini Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3-18 mwaka huu.

Timu zimepangwa katika Kanda Saba ambapo mshindi wa kila kanda pamoja na mwenyeji Msumbiji ndiye atakayekwenda kushiriki fainali hizo. Tanzania iko Kanda ya Tano pamoja na timu za Eritrea, Kenya na Uganda.

Iwapo U23 itaitoa Uganda itacheza na mshindi kati ya Eritrea na Kenya. Mechi ya kwanza itachezwa ugenini kati ya Juni 24-26 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa kati ya Julai 8-10 mwaka huu. U23 iko kambini Bamba Beach, Kigamboni ikiwa chini ya Kocha Kihwelo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Monday, April 11, 2011

18 PLAYERS NAMED FOR FRIENDLY AGAINST MOZAMBIQUE

GOALKEEPERS:
Shabani Kado (Mtibwa Sugar) and Shaaban Dihile (JKT Ruvu).

DEFENDERS:
Shadrack Nsajigwa (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub ‘Cannavaro’
(Yanga), Amir Maftah (Simba), Juma Nyoso (Simba) and Kigi Makasi (Yanga).

MIDFIELDERS:
Nurdin Bakari (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Jabir Aziz (Azam), Ramadhan Chombo ‘Redondo’ (Azam) and Mwinyi Kazimoto (JKT Ruvu).

ATTACKERS:Machaku Salum (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngasa (Azam), Mohamed Banka (Simba), John Bocco (Azam) and Mbwana Samata (Simba).

*The following will be called for CAN 2012 qualifiers match against CAR;Juma
Kaseja (Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) and Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden).

Boniface Wambura
Media Officer

MAPATO SIMBA v MAJIMAJI

Mechi namba 132 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Majimaji iliyochezwa Aprili 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 19,799,000.

Mapato hayo ni kutokana na watazamaji 4,611 waliolipa kutazama mechi hiyo.
Viingilio katika pambano hilo vilikuwa sh. 15,000 kwa VIP A, sh. 10,000 VIP B na sh. 7,000 VIP C. Sehemu nyingine zilizobaki kiingilio kilikuwa sh. 3,000.

Baada ya kuondoa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 3,020,186.44 fedha iliyobaki kwa mgawanyo kwa pande zote husika ni sh.
16,778,813.56.

Gharama za awali za mchezo kabla ya mgawanyo ni sh. 5,366,605.36. Gharama hizo zinahusisha asilimia 10 ya uwanja, mjenzi wa uwanja kampuni ya Beijing
Construction, uchapaji tiketi, nauli za ndani na malazi kwa kamishna na waamuzi, jichangie kwa kila klabu na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), umeme, ulinzi na usafi.

Mgawanyo baada ya gharama hizo kila timu ilipata sh. 1,253,817.91, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 417,939.30, gharama za mchezo sh. 417,939.30, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 37,994.48, DRFA sh. 189,972.41 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 227,966.89.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Sunday, April 10, 2011

Jan Poulsen kuongea na waandishi wa habari jumatatu

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen atakuwa na mkutano na waandishi wa habari. Siku: Jumatatu Tarehe: Aprili 11, 2011 Muda: Saa 6 kamili mchana Mahali: TFF Regards Boniface Wambura TFF Media Officer

MAPATO U23 VS CAMEROON

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Aprili 10, 2011


Mechi ya mchujo ya michuano ya Olimpiki kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ya umri wa chini ya miaka 23 na Cameroon iliyofanyika Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 31,681,000.


Baada ya kuondoa sh. 4,832,694.92 ambayo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), fedha iliyobaki kwa ajili ya mgawanyo ni sh. 26,848,305.08. Gharama za awali za mechi kabla ya mgawanyo zinazojumuisha kamishna na waamuzi, uchapaji tiketi, ulinzi, usafi wa uwanja, umeme na kampuni ya Beijing Construction ya China ni sh. 17,458,000.


Mgawanyo wa mapato baada ya kuondoa gharama za awali ni sh. 939,030.51 ambayo ni asilimia 10 ya gharama za mchezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 469,515.25, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 7,042,728.81 na asilimia 10 ya uwanja ni sh. 939,030.51.


Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 10,000 kwa VIP A, sh. 5,000 kwa VIP B na VIP C wakati viti vya kijani, bluu na rangi ya chungwa ilikuwa sh. 1,000. MPINZANI WA U23 Timu itakayocheza na U23 katika raundi ya pili ya michuano ya mchujo ya Olimpiki itajulikana Aprili 13 mwaka huu wakati shughuli ya upangaji ratiba itakapofanyika makao makuu ya CAF jijini Cairo, Misri.


U23 ni moja ya timu 16 zilizofuzu kwa ajili ya raundi ya pili ambayo mechi za kwanza zitachezwa kati ya Juni 3, 4 na 5 na zile za marudiano kufanyika kati ya Juni 17, 18 na 19 mwaka huu. Afrika katika michezo hiyo ya Olimpiki itakayofanyika mwakani jijini London, Uingereza itawakilishwa na timu tatu. Nafasi ya nne itagombewa na timu za Afrika na Asia zilizoshika nafasi ya nne katika mchujo katika kwenye mabara yao. Timu hizo zitacheza mechi hiyo (play off) Aprili 12 mwakani jijini London. Boniface Wambura Ofisa Habari

Friday, April 8, 2011

MAREKEBISHO YA KANUNI ZA UCHAGUZI

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF ibara ya 34 (k), Kamati ya Utendaji ya TFF imefanya marekebisho madogo ya Kanuni za Uchaguzi za TFF na za Wanachama wake. Mabadiliko haya yamelenga:

1 Kuainisha kwa uwazi idadi ya siku zinazotakiwa kuzingatiwa na Kamati za Uchaguzi kwa kila shughuli muhimu ya mchakato wa uchaguzi ili kuondoa uwezekano wa kuchelewesha utekelezaji wa hatua mbalimbali za msingi za mchakato wa uchaguzi.

2 Kuweka wazi sifa na matakwa kwa wajumbe wa Kamati za Uchaguzi katika ngazi ya TFF, wanachama wa TFF na Wilaya, kwa lengo la kuondoa ukiritimba wa uongozi na mzozo wa masilahi (Conflict of interest) na pia kubainisha wazi matakwa ya kutofungamana (neutrality) na shughuli za utendaji kwa wajumbe wa Kamati za uchaguzi, ili kuimarisha uwajibikaji katika vyombo vya usimamiaji wa upatikanaji wa viongozi bora wa soka nchini.

Kwa mujibu wa marekebisho yaliyofanyika, Wajumbe wa Kamati za uchaguzi hawataruhusiwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji TFF, Kamati za Utendaji za wanachama wa TFF na za vyama vya mpira wa miguu vya wilaya. Aidha wajumbe wa Kamati za uchaguzi kwa ngazi yoyote hawataruhusiwa kuwa wajumbe wa Kamati za Uchaguzi wa ngazi za chini yake. Pia Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya mwanachama wa TFF hataruhusiwa kuwa mjumbe wa kamati ya uchaguzi ya mwanachama mwingine wa TFF kwa wakati mmoja.

3 Kuondoa utata (ambiguity) katika matakwa ya sifa ya elimu kwa wagombea uongozi katika vyama vya soka nchini. Wagombea uongozi kwa nafasi zote za kuchaguliwa wanatakiwa kuwa na cheti cha kidato cha nne au kuwa na elimu ya kiwango cha zaidi ya kidato cha nne, kwa mujibu wa katiba.

4 Kuweka wazi mtiririko wa ukataji rufaa kutoka ngazi ya Wilaya hadi Taifa (TFF) kwa kuzipa mamlaka Kamati za Uchaguzi za Mikoa kusikiliza rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati za uchaguzi za Wilaya.

5 Kuainisha viwango vya ada za fomu za kuomba uongozi na za rufaa kwa ngazi za Wilaya, Mikoa na TFF.

Kamati inawataka wanachama wote wa TFF kuteua wajumbe wa Kamati za Uchaguzi na kufanya chaguzi zake kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF.


Deogratias Lyatto

MWENYEKITI

KAMATI YA UCHAGUZI -TFF

twiga stars yataja majina ya waliochaguliwa leo


Kocha wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars),Charles Boniface ametangaza majina ya wachezaji 26 watakaoanza mazoezi Aprili 11 mwaka huu kwa ajili ya mechi yao ya mchujo ya michezo ya Afrika (All Africa Games) dhidi ya Sudan.

Wachezaji walioitwa ni Asha Rashid (Mburahati Queens), Neema Jacob (Simba
Queens), Sophia Mwasikili (Sayari), Fadhila Hamad (Uzuri), Irene Matowo
(Mburahati Queens), Hellen Tolla (JKT), Mwanahamisi Shurua (Mburahati Queens),Fatuma Jawadu (Sayari), Fatuma Swalehe (Simba Queens), Maimuna Mkane (JKT),Pulkelia Charaji (Sayari), Fatuma Makusanya (Simba Queens) na Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens).

Wengine ni Fridiana Daudi (JKT), Fatuma Salum (Mburahati Queens), Mwajuma Abdillah (Tanzanite), Mariam Fakil (Tanzanite), Mwasiti Selemani (Tanzanite),Aziza Lugendo (Mburahati Queens), Suzana Komba (TMK), Rukia Hamisi (Evergreen),Pendo Juma (Evergreen), Zena Khamis (Mburahati Queens), Tatu Said (Umonga Sekondari, Dodoma), Mwanaidi Khamis (Uzuri Queens) na Zena Said (Uzuri Queens).

Kwa siku kumi za kwanza, Twiga Stars itafanya mazoezi Uwanja wa Karume kwa wachezaji kutokea nyumbani (off camp) na baada ya hapo itaingia rasmi kambini Aprili 20 mwaka huu.

Twiga Stars itacheza mechi yake ya kwanza ugenini Aprili 30 mwaka huu, wakati ya marudiano itachezwa Mei 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Twiga Stars ikiitoa Sudan itakuwa imefuzu kwa michezo ya All Africa Games ambayo itafanyika Septemba mwaka huu jijini Maputo, Msumbiji.

MAPATO MECHI YA AFRICAN LYON vs YANGA


Mechi namba 125 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya African Lyon na Yanga iliyochezwa Aprili 7 mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam imeingiza sh. 22,252,000.

Mapato hayo ni kutokana na watazamaji 4,476 waliolipa kutazama mechi hiyo.
Viingilio katika pambano hilo vilikuwa sh. 15,000 kwa VIP, sh. 8,000 Jukwaa
Kubwa, sh. 5,000 Jukwaa la Kijani n ash. 3,000 Mzunguko.

Baada ya kuondoa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 3,394,372.88 fedha iliyobaki kwa mgawanyo kwa pande zote husika ni sh. 18,857,627.12.

Jumla ya gharama za awali za mchezo ni sh. 5,185,200 wakati kila timu ilipata
sh. 4,101,728.14. Uwanja sh. 1,367,242.71, TFF sh. 1,367,242.71, gharama za mchezo sh. 1,367,242.71, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 136,724.27, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 546,897.08 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 683,621.36.

Thursday, April 7, 2011

MAPATO SIMBA v JKT RUVU

Kikosi cha Simba SC
Kikosi cha JKT RUVU.

Picha zote na Maktaba.

Mechi namba 119 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na JKT Ruvu iliyochezwa Aprili 6 mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam imeingiza sh. 21,106,000.


Mapato hayo ni kutokana na watazamaji 4,264 waliolipa kutazama mechi hiyo.
Viingilio katika pambano hilo vilikuwa sh. 15,000 kwa VIP, sh. 8,000 Jukwaa
Kubwa, sh. 5,000 Jukwaa la Kijani n ash. 3,000 Mzunguko.

Baada ya kuondoa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 3,219,559 fedha iliyobaki kwa mgawanyo kwa pande zote husika ni sh.17,886,441.

Jumla ya gharama za awali za mchezo ni sh. 2,275,000 wakati kila timu ilipata
sh. 4,683,252. Uwanja sh. 1,561,084, TFF sh. 1,561,084, gharama za mchezo sh.
1,561,084, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 156,108, Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 624,433 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 780,542.

Wednesday, April 6, 2011

Umri wa Ngassa wazua gumzo U23

Mchezaji Mrisho Ngasa akiwa katika moja ya mechi zake za kimataifa.


Kocha Jamhuri Kihwelo ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi chake cha U23 kwa lengo la kukiimarisha kabla ya mechi ya marudiano ya michuano ya Olimpiki dhidi ya Cameroon itakayofanyika Jumamosi (Aprili 9 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji hao ni Kigi Makasi kutoka Yanga, David Luhende (Kagera Sugar), Jabir Aziz (Azam), Kelvin Chale (Simba), Ali Lundenga (Kagera Sugar), Mrisho Ngasa (Azam) na Juma Abdul (Mtibwa Sugar).

Baada ya uamuzi huo wa kocha, baadhi ya washabiki na vyombo vya habari
vimeonesha mashaka juu ya umri wa Ngasa. Kwanza TFF inapenda kuweka wazi kuwa umri chini ya miaka 23 ndiyo sifa ya msingi ya kuchezea timu hiyo.

Hivyo uamuzi wa kocha kuita wachezaji hao mbali ya vigezo vingine, cha umri pia kimezingatiwa. Umri wa Ngasa aliyezaliwa Aprili 12, 1989 ni miaka 22. Wachezaji wengine walioongezwa na tarehe zao za kuzaliwa ni Makasi (Februari 2, 1990), Luhende (Januari 21, 1989), Aziz (Januari 1, 1989), Chale (Juni 19, 1992), Lundenga (Septemba 12, 1990) na Abdul (Novemba 10, 1992).


Boniface Wambura
Ofisa Habari

Tuesday, April 5, 2011

SABA WAONGEZWA U23

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 5, 2011

Kocha Jamhuri Kihwelo ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi chake cha U23 kwa ajili ya mechi ya marudiano ya mchujo ya michuano ya Olimpiki dhidi ya Cameroon itakayochezwa Jumamosi (Aprili 9 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji hao ni Kigi Makasi kutoka Yanga, David Luhende (Kagera Sugar), Jabir
Aziz (Azam), Kelvin Chale (Simba), Ali Lundenga (Kagera Sugar), Mrisho Ngasa
(Azam) na Juma Abdul (Mtibwa Sugar).

VIINGILIO U23 v CAMEROON
Viingilio katika mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni ni kuanzia sh.
1,000. Mashabiki watakaokaa viti vya kijani, bluu na rangi ya chungwa (orange)
ndiyo watakaolipa kiasi hicho wakati VIP B na VIP C kiingilio kitakuwa sh.
5,000. Jukwaa la VIP A lenye viti 745 kiingilio kitakuwa sh. 10,000. Tiketi
zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mechi.

Tiketi zitauzwa katika vituo vya OilCom Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin
Mkapa, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio, Bigbon Msimbazi (Kariakoo) na Uwanja wa Uhuru. Mechi itaanza saa 10 kamili. Cameroon imewasili nchini jana saa 5.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways ikiwa na wachezaji 23 na imefikia Paradise City Hotel.

Mwamuzi wa mechi hiyo ni Aime Ndayisenga akisaidiwa na Desire Gahungu,
Jean-Claude Birumushahu na Athanase Niyongabo, wote kutoka Burundi. Kamishna wa mchezo huo ni Charles Masembe kutoka Uganda.

FIFA YAISIMAMISHA BOSNIA-HERZEGOVINA
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) limeisimamisha
Bosnia-Herzegovina kuanzia Aprili Mosi mwaka huu baada ya Mkutano Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu la nchi hiyo (FFBH) kutopitisha Katiba yake
iliyofanyiwa marekebisho kwa kuzingatia matakwa ya FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ulaya (UEFA).


Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke iliyotumwa kwa
wanachama wake, FFBH inapoteza haki zote ilizokuwa nazo kutokana na uanachama wake kwa Shirikisho hilo hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine.

Kutokana na kusimamishwa huko, wanachama wote wa FIFA hawatakiwi kushirikiana na FF BH katika masuala yoyote isipokuwa yale yanayohusu mchezaji binafsi. Hatua hiyo imefikiwa kutoka na uamuzi uliofikiwa Oktoba 28 mwaka jana na Kamati ya Utendaji ya FIFA kuwa FFBH iwe imetekeleza matakwa hayo kufikia Machi 31 mwaka huu.


Boniface Wambura
Ofisa Habari

makamu wa rais akutana na dr asha-rose migiro na ujumbe wake leo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal kulia, akizungumza na Ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Dk. Asharose Migiro wakati Ujumbe huo ulipofika Ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu Dar es salaam leo kwa ajili ya mazungumzo.
Picha na mdau Amour Nassor wa VPO.

VIINGILIO U23 v CAMEROON

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 5, 2011

VIINGILIO U23 v CAMEROON
Viingilio katika mechi ya marudiano ya mchujo ya michuano ya Olimpiki kati ya
timu ya Taifa ya Tanzania ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 23 dhidi ya
Cameroon itakayochezwa Jumamosi (Aprili 9 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam ni kuanzia sh. 1,000.

Mashabiki watakaokaa viti vya kijani, bluu na rangi ya chungwa (orange) ndiyo
watakaolipa sh. 1,000 wakati VIP B na VIP C kiingilio kitakuwa sh. 5,000. Jukwaa
la VIP A lenye viti 745 kiingilio kitakuwa sh. 10,000. Tiketi zitaanza kuuzwa
siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mechi.

Tiketi zitauzwa katika vituo vya OilCom Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin
Mkapa, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio, Bigbon Msimbazi (Kariakoo)
na Uwanja wa Uhuru. Mechi itaanza saa 10 kamili.

Cameroon imewasili nchini jana saa 5.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways ikiwa
na wachezaji 23 na imefikia Paradise City Hotel.

FIFA YAISIMAMISHA BOSNIA-HERZEGOVINA
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) limeisimamisha
Bosnia-Herzegovina kuanzia Aprili Mosi mwaka huu baada ya Mkutano Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu la nchi hiyo (FFBH) kutopitisha Katiba yake
iliyofanyiwa marekebisho kwa kuzingatia matakwa ya FIFA na Shirikisho la Mpira
wa Miguu la Ulaya (UEFA).


Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke iliyotumwa kwa
wanachama wake, FFBH inapoteza haki zote ilizokuwa nazo kutokana na uanachama
wake kwa Shirikisho hilo hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine.

Kutokana na kusimamishwa huko, wanachama wote wa FIFA hawatakiwi kushirikiana na
FF BH katika masuala yoyote isipokuwa yale yanayohusu mchezaji binafsi. Hatua
hiyo imefikiwa kutoka na uamuzi uliofikiwa Oktoba 28 mwaka jana na Kamati ya
Utendaji ya FIFA kuwa FFBH iwe imetekeleza matakwa hayo kufikia Machi 31 mwaka
huu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Friday, April 1, 2011

MAPATO MECHI YA SIMBA NA KAGERA SUGER HAYA HAPA

Mchezaji wa timu ya Simba Emmanuel Okwi (kushoto) akichuana vikali na beki wa timu ya Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa Machi 29 kwenye uwanja wa uhuru jijini Dar.

Mechi namba 122 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera Sugar iliyochezwa Machi 29 mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam imeingiza sh. 23,637,000.

Baada ya kuondoa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 3,605,644 fedha iliyobaki kwa mgawanyo kwa pande zote husika ni sh. 20,031,355.93.

Jumla ya gharama za awali za mchezo ni sh. 3,635,600 wakati kila timu ilipata sh. 4,918,726.78. Uwanja sh. 1,639,575.59, TFF sh. 1,639,575.59, gharama za mchezo sh. 1,639,575.59, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 163,957.56, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 655,830.24 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 819,787.80.

MKUTANO MKUU WA TFF WAICHANGIA TAIFA STARS

Baadhi ya Wajumbe waliohudhulia Mkutano mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF)

Timu ya Taifa (Taifa Stars) ambayo inashiriki michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) zitakazochezwa Gabon- Equatorial Guinea mwakani imechangiwa sh. 1,980,000.

Fedha hizo kwa Taifa Stars iliyo kundi D pamoja na Morocco, Algeria na Jamhuri ya Afrika ya Kati zilichangwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uliofanyika Machi 26 na 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wa Mkutano huo walishuhudia mechi kati ya Taifa Stars na Jamhuri ya Afrika ya Kati iliyochezwa Machi 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Walichanga fedha hizo kuipongeza Stars baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation