Monday, October 28, 2013

JAMAL MALINZI NDIYE RAIS MPYA WA TFF

Jamal Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo kwa kupata kura 73 kati ya kura 126 zilizopigwa, dhidi ya mpinzania wake Athumani Nyamlani aliyepata kura 52 kwenye kinyang'anyiro hicho kilichohitimishwa usiku wa kuamkia leo katika jengo la NSSF la Waterfront jijini Dar es salaam.

Malinzi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha soka cha mkoa wa Kagera ameshinda uchaguzi huo ikiwa ni mara yake ya pili kugombea baada ya kushindwa na Rais wa zamani wa TFF Leodgar Chillah tenga mwaka 2008.Nafasi ya Makamu wa Rais imenyakuliwa na Wallace Kiria aliyemshinda Ramadhani Nasib kwa kura 67 dhidi ya 52, wakati mgombea mwingine katika nafasi hiyo Imani Mahugila Madega kapata kuta 6. 

Katika nafasi za Ujumbe; Kanda ya 13; kiungo wa zamani wa Simba SC Wilfred Kidau amepata kura 60 na kuwashinda Muhsin Said kura 50, Omar Abdulkadir kura 10 na Alex Kabuzelia kura nne. Kanda 12; Khalid Mohamed Abdallah amepata kura 69 na kumshinda Davies  Mosha aliyepata kura 54. 

 Kanda ya 11 Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amepata kura 78 na kuwashinda Riziki Majala kura tano, Twahir Njoki kura mbili, Juma Pinto kura 26 na Farid Mbaraka kura 14, Kanda ya 10 ameshinda Hussein Mwamba aliyepata kura 63, huku Charles Komba akipata nne na Stewart Nasima 58. 

 Kanda ya tisa Othman Kambi aliyepata kura 84 yeye amewashinda Francis Bulame kura 30, wakati James Mhagama aliyepata 93 amemshinda Zafarani Damoda aliyepata kura 11 na Kanda ya nane, Ngube Kiondo amepata kura 73 amemshinda Ayoub Nyaulingo kura 52. 

 Kanda ya Tano, Ahmed Iddi Mgoyi aliyepata kura 92 amemshinda Yussuf Kitumbo aliyepata kura 34, wakati Kanda Omar Walii Ali amepata kura 53 dhidi ya 19 za Ally Mtumwa. 

Eley Mbise amepata kura 51 dhidi ya 53 kura 57 za Lamanda Swai. Mbasha Matutu aliyepata kura 63, amembwaga Vesastis Ligano aliyepata kura 61, wakati Vedastus Lufano aliyepata kura 51, amewashinda Jumbe Odesa Magati kura 11, Mugisha Galibona kura 24 na Samuel Nyalla kura 39 na Kanda namba moja, Karilo Samson hakuwa na mpizani akapita moja kwa moja.
Rais mpya wa TFF Jamal Malinzi akiwa na Dream Team yake baada ya uchaguzi
Rais Mstaafu wa TFF LEodegar Chilla Tenga akimkabidhi mikoba Rais Mpya Jamali Malinzi akkisaidiwa na katibu mkuu Angetille Osiah.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa miguu nchini aliyemaliza muda wake,Leodger Tenga (kushoto) akimkabidhi Mpira Rais Mpya wa shirikisho hilo,Jamal Malinzi mara baada ya kutangazwa mshindi katika Uchaguzi uliofanyika jana na kumalizika usiku wa kuamkia leo,ambapo alimshinda mpinzani wake,Athuman Nyamlani kwa kura 73.uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Water Front jijini Dar es salaam.Katika uchaguzi huo nafasi ya Umakamu wa Rais ilichukuliwa na Walace Karia ambaye alifanikiwa kuwagaragaraza wapinzani wake Imani Madega na Ramadhan Nassib.
Rais Mpya wa Shirikisho la Mpira wa miguu nchini,Jamal Malinzi akizungumza machache na Wajumbe wa Uchaguzi huo mara baada ya kutangazwa Mshindi wa nafasi ya Urais wa TFF,usiku wa kuamkia leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Water Front,jijini Dar es Salaam.Kulia ni Makamu Mpya wa Rais wa TFF,Walace Karia.
Rais Mpya wa Shirikisho la Mpira wa miguu nchini,Jamal Malinzi akipongezana na Makamu Mpya wa Rais wa TFF,Walace Karia mara baada ya kuibuka Kidedea.
Shangwe,Nderemo na Vifijo vilitawala kwenye eneo la Ukumbi wa Water Front jijini Dar es Salaam,mara baada ya Washindi kupatikana.Picha na FullShangwe Blog.

Sunday, March 25, 2012

SIMBA YASHINDA BAO 2 - 0 DHIDI YA ES SATIF UWANJA WA TAIFA LEO

 Ubao wa Matangazo ukionyesha matokeo ya mchezo wa leo
  Kikosi cha Simba.
 Kikosi cha Es Satif
 Marefarii na Manahodha wa timu zote mbili.
 Mkono wa kheri kabla ya mtanange kuanza.
 Mshambuliaji wa Timu ya Simba,Salum Machaku (kulia) akijiandaa kuachia shuti kali kuelekea langoni mwa timu ya Es Satif katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho uliochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Simba imeshinda bao 2 - 0.
 Mshambuliaji wa Simba,Emmanuel Okwi (kulia) akimtoka beki wa timu ya Es Satif ya nchini Argeria,Farouk Belkaid katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho uliomalizika muda mfupi uliopita kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Simba imeshinda bao 2 - 0,mabao yaliyopatikana kipindi cha pili cha mchezo kupitia kwa Emmanuel Okwi na Haruna Moshi.
 Ameir Maftah wa timu ya Simba (kulia) akiachia shuti kali kuelekea langoni mwa timu ya Es Satif.
 Beki wa Es Satif (alielala chini) akiondosha hatari langoni mwake wakati Salum Machaku akitaka kujaribu kufunga goli.
 Holaaaaaa..........
 Hatari langoni mwa Es Satif.
 Waziri Mkuu mstaafu,Mh. Fredrick Sumaye (mwenye suti),Waziri wa Afrika Mashariki,Mh. Samuel Sitta (kulia),Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe pamoja na Mbunge wa Tabora Mjini,Mh. Aden Rage wapo uwanjani hapa kuisapoti timu ya Simba.
 Kocha wa Timu ya Shimba,Milovan Cirkovic (kushoto) akipeana mkono na Kocha wa timu ya Es Satif,Alain Geiger mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho,uliochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijinin Dar es Salaam.Simba imeshinda bao 2 - 0.
Mashabiki wa timu zote mbili wanavyoonekana.
Mashabiki wa Es Satif wakiwa na huzuni iliyopitiliza.
Onyo kali uwanjani.
 Mashabiki wa Simba wakiwa wamefurika uwanjani hapa.

Tuesday, August 23, 2011

Release No. 80 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 23, 2011


RATIBA YA LIGI KUU MZUNGUKO WA KWANZA
Baada ya Serikali kuufunga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya marekebisho, Yanga na Simba ambazo awali zilikuwa zimeruhusiwa kutumia uwanja huo kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zililazimika kutafuta viwanja vipya. Simba imehamia Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Yango iko Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
 
Licha ya timu hizo kupata viwanja vipya ratiba itabaki kama ilivyotolewa awali. Mechi za Simba zilizokuwa zichezwe Uwanja wa Taifa sasa zitachezwa Mkwakwani wakati za Yanga zitachezwa Jamhuri. Kutokana na mabadiliko hayo ratiba inasomeka kuwa Septemba 7 mwaka huu Coastal Union v Moro United (Mkwakwani) na pia Simba v Villa Squad (Mkwakwani). Mechi ya Simba v Villa Squad imesogezwa mbele kwa siku moja ambapo sasa itachezwa Septemba 8 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
 
MCHEZAJI CASTORY MUMBARA
TFF imeshindwa kumpa leseni Castory Mumbara ambaye ameombewa usajili katika timu ya Toto Africans kutokana na kutokuwa na Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) ambayo inatakiwa kutolewa kupitia mfumo wa mtandao wa Transfer Matching System (TMS).
 
Ikumbukwe kuwa Mumbara alikuwa akichezea timu ya Himalayan Sharpa ya Nepal ambapo alikwenda huko baada ya TFF kumpatia ITC. Hivyo ili aichezee Toto Africans, klabu hiyo ilipaswa kumuombea hati hiyo kupitia mtandao wa TMS baada ya kufanya mawasiliano na Himalayan Sharpa.
 
Muda wa usajili ulimalizika Julai 31 mwaka huu, hivyo Toto Africans kwa sasa haiwezi kumtumia mchezaji huyo badala yake inatakiwa kusubiri dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa tena Novemba mwaka huu. TFF iliendesha mafunzo ya kutumia mfumo wa TMS kwa watendaji wote wa klabu za Ligi Kuu ikiwemo Toto Africans.
 
MECHI YA STARS v ALGERIA
Mechi hiyo namba 103 ya mchujo kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Equatorial Guinea na Gabon itachezwa nchini Septemba 3 mwaka huu.
 
Bado tunasubiri majibu ya ombi letu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo la kuturuhusu kutumia Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo.
 
ALL AFRICA GAMES
Mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Tanzania ni miongoni mwa waamuzi 32 (waamuzi wa kati na wasaidizi) walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha michezo ya All Africa Games itakayofanyika Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3-18 mwaka huu. Kati ya hao, 16 ni wanaume na 16 ni wanawake.
 
Kanyenye ni mmoja kati ya waamuzi watatu kutoka  ukanda wa CECAFA- Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati walioteuliwa kuchezesha michezo hiyo. Wengine ni mwamuzi wa kati wa kike kutoka Uganda, Nabikko Ssemambo na mwamuzi msaidizi wa kike kutoka Ethiopia, Trhas Gebreyohanis.
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Monday, August 22, 2011

Release No. 79 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 22, 2011

Sendeu


Rage
RAGE, SENDEU KAMATI YA NIDHAMU
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepeleka mashtaka mbele ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi dhidi ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Agosti 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine iliiagiza Sekretarieti kupeleka mashtaka hayo kutokana na kauli za viongozi hao kabla ya mechi ya Yanga na Simba iliyochezwa Agosti 17 mwaka huu.
Rage alikaririwa na vyombo vya habari kuwa Simba haitapeleka timu uwanjani kama mchezaji wake Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati hataruhusiwa kucheza, na kuwa ofisa mmoja wa TFF ndiye kikwazo kwa uhamisho wa mchezaji huyo.
Naye Sendeu kupitia vyombo vya habari alikaririwa kuwa Yanga haitaingiza timu uwanjani hadi itakapolipwa sh. milioni 16 inazoidai TFF ingawa deni hilo halikuwa na uhusiano na mechi hiyo ya Ngao ya Jamii.
Kauli hizo si tu zililenga kuvuruga mechi hiyo kwa kuwachanganya mashabiki, bali zilikuwa za kudhalilisha mchezo wa mpira wa mpira wa miguu.
Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi inayoongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) mstaafu Alfred Tibaigana itakuwa na kikao Agosti 28 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine itajadili mashtaka dhidi ya viongozi hao.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Saturday, August 20, 2011

Release No. 78 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 20, 2011

AFRICAN LYON KULIPA WACHEZAJI KWA MAKATO

Timu ya African Lyon imeomba kuwalipa kwa makato ya mlangoni wachezaji wake wawili wanaoidai; Godfrey Komba na Abdul Masenga ambao ilikatiza mikataba yao msimu uliopita. Awali Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliiagiza Lyon kuwalipa wachezaji hao kufikia Agosti 17 mwaka huu vinginevyo isingeruhusiwa kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom inayoanza leo (Agosti 20 mwaka huu).

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliitaka Lyon ithibitishe kwa maandishi kuwa itakatwa kwenye mapato yake ya mlangoni katika mechi hadi deni la wachezaji hao litakapomalizika. Lyon imetekeleza maagizo hayo, hivyo imeruhusiwa kucheza mechi yake ya leo (Agosti 20 mwaka huu) dhidi ya Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Hivyo Lyon itakatwa katika mechi yake ya leo ili kulipa deni hilo. Kama fedha ilizopata katika mgawo hazitatosha kulipa deni hilo itakatwa sehemu iliyobaki katika mechi inayofuata.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji katika kikao chake cha Januari 7 mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa kiliiagiza Lyon iwalipe wachezaji hao baada ya kusitisha mikataba yao nje ya taratibu za kimikataba. Masenga na Komba kila mmoja anadai sh. milioni 4.3.

Wachezaji hao wataarifiwa juu ya utaratibu wa malipo yao ambapo TFF ndiyo itakayofanya makato kwa niaba yao.

FIFA YARUHUSU ITC YA KAGO ITOLEWE

Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) limeruhusu Shirikisho la Mpira wa Miguu Jamhuri ya Afrika ya Kati kutoa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Gervais Anold Kago aliyejiunga na timu ya Simba kutoka Olympic Real de Bangui ya huko.

FIFA imeruhusu ITC itolewe baada ya kubaini kuwa Simba ilituma maombi ya kuomba hati hiyo ndani ya muda uliopangwa, lakini CAR ilishindwa kufanyia kazi. Hivyo kinachosubiriwa sasa ni CAR kutuma ITC hiyo.

Licha ya FIFA kuagiza hivyo, TFF imeitaka Simba kukata jina moja kati ya sita ya wachezaji wa kigeni ilionao katika orodha yake. Kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom inaruhusu timu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi watano.

Wachezaji wa kigeni ambao Simba ina mikataba yao ni Derrick Walulya, Emmanuel Okwi, Felix Sunzu, Gervais Kago, Patrick Mafisango na Jerry Santo.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji wakati ikipitia usajili iliagiza kuwa Walulya ambaye Simba ilisema imemuacha ni mchezaji wake kwa vile bado ina mkataba nayo. Hivyo inachotakiwa kufanya Simba ni kuvunja mkataba wa mchezaji mmoja ili kubaki na watano.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Friday, August 19, 2011

Release No. 77 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 19, 2011



MSIMU MPYA LIGI KUU YA VODACOM
Msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom 2011/2012 unaanza kesho (Agosti 20 mwaka huu) ambapo timu 10 kati ya 14 zinazoshiriki katika ligi hiyo zitakuwa viwanjani. Mechi za kesho ni Coastal Union v Mtibwa Sugar (Mkwakwani, Tanga), Kagera Sugar v Ruvu Shooting (Kaitaba, Bukoba), Toto Africans v Villa Squad (Kirumba, Mwanza) na Polisi Dodoma v African Lyon (Jamhuri, Dodoma).
 
Mechi nyingine ni Azam v Moro United itakayochezwa Chamazi, Dar es Salaam wakati mechi za Jumapili (Agosti 21 mwaka huu) ni Oljoro JKT v Simba (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), na Yanga watakaokuwa wenyeji wa JKT Ruvu.
 
WAAMUZI WA KATI
Waamuzi wa kati (centre referees) 16 wameteuliwa kuchezesha Ligi Kuu. Waamuzi hao ni Ronald Swai (Arusha), Isihaka Shirikisho (Tanga), Peter Mujaya (Mwanza), Amon Paul (Mara), Mathew Akrama (Mwanza), Ibrahim Kidiwa (Tanga), Dominic Nyamisana (Dodoma), David Paul (Mtwara), Hashim Abdallah (Dar), Martin Saanya (Morogoro), Orden Mbaga (Dar), Kennedy Mapunda (Dar), Israel Mujuni (Dar), Alex Mahagi (Mwanza), Abdallah Kambuzi (Shinyanga) na Thomas Mkombozi (Kilimanjaro).
 
Pia wameteuliwa waamuzi wa akiba (reserve referees) sita ambao watatumika wakati wowote watakapohitajika. Waamuzi wasaidizi (assistant referees) walioteuliwa kuchezesha ligi ni 34. Kwa upande wa waamuzi wasaidizi wa akiba walioteuliwa ni kumi. Hivyo jumla ya waamuzi watakaotumika kwenye ligi hiyo ni 50.
 
MAKAMISHNA WA MECHI
Jumla ya makamishna (match commissioners) 24 wameteuliwa kusimamia mechi za ligi hiyo. Kati ya hao 20 ni wa zamani na wanne ni wapya. Makamishna wapya ni Charles Ndagala, Victor Mwandike, Godbless Kimaro na Hamis Tika.
 
Makamishna wa msimu uliopita walioteuliwa tena ni Hamis Kissiwa, David Lugenge, Abdallah Mitole, Charles Komba, George Komba, Jimmy Lengwe, Amri Kiula, James Mhagama, Fulgence Novatus, Pius Mashera, Michael Bundara, Gabriel Gunda, Mohamed Nyange, Mwijage Rugakingira, Arthur Mambeta, Paul Opiyo, Edward Hiza, Salim Singano, William Chibura na Omary Mwamela.
 
Uteuzi wa makamishna kama ilivyo kwa waamuzi ulifanyika baada ya kuhudhuria kozi na kufanya mitihani. Kwa upande wa makamishna ambao hawakufanya vizuri, watalazimika kurudia mitihani kabla ya kuteuliwa tena.
 
NAULI KWA TIMU ZINAZOSHIRIKI LIGI
Kila timu inayoshiriki ligi itapata jumla ya sh. milioni 26.3. Fedha hizo zitatolewa kwa awamu tano tofauti kuanzia mwezi huu. Agosti kila timu itapata sh. 4,732,142, Septemba (sh. 4,732,142), Oktoba (sh. 5,622,321), Januari (sh. 5,622,321) na Machi (sh. 5,622,321).
 
Jumla ya fedha kutoka kwa mdhamini wa ligi, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ambazo zitatumika kwa ajili ya nauli kwa timu zote katika msimu mzima ni sh. 368,637,458.
 
MECHI YA STARS, ALGERIA
Tumeiandikia barua Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuomba iruhusu mechi ya mchujo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Equatorial Guinea na Gabon kati ya Taifa Stars na Algeria (Desert Warriors) ichezwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Ombi letu limetokana na ukweli kuwa tulishaliarifu Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) miezi mitatu iliyopita kuwa mechi hiyo itachezwa katika uwanja huo. Taarifa hiyo pia tuliipa Algeria ambayo imeshatuma ujumbe wake kukagua hoteli ambayo timu yao itafikia.
 
Kwa upande wa CAF uamuzi wa kubadili uwanja hivi sasa maana yake kuwa itatupiga faini, lakini vilevile TFF tutalazimika kuingia gharama za kusafirisha kwa ndege timu zote mbili pamoja na waamuzi kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo.
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Thursday, August 18, 2011

Release No. 76 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 18, 2011


STARS, ALGERIA KUCHEZA MWANZA
Mechi ya mchujo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) zitakazofanyika mwakani nchini Equatorial Guinea na Gabon katika ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Algeria (Desert Warriors) itachezwa Septemba 3 mwaka huu jijini Mwanza.
 
Awali tulipanga mechi hiyo ichezwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Lakini uamuzi wa kuihamishia Mwanza umefanyika baada ya jana kupata barua kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ikitufahamisha kuwa Uwanja wa Taifa hautatumika tena kwa sasa. Kwa mujibu wa Wizara, uwanja huo utakuwa katika matengenezo baada ya kuharibika wakati wa michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita.
 
YANGA, SIMBA NAZO KUATHIRIKA
Uamuzi huo wa uwanja kufungwa kwa ajili ya matengenezo pia umeziathiri klabu za Yanga na Simba ambazo zilikuwa zimekubaliwa timu zao zitumie kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom ambayo inaanza kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu.
 
Tayari leo (Agosti 18 mwaka huu) tumeziandikia rasmi klabu za Simba na Yanga kuzifahamisha kuhusu uamuzi huo wa Wizara, hivyo kuzitaka zitafute viwanja vingine kwa ajili ya mechi zao za ligi.
 
Hatua hiyo ya uwanja kufungwa, itailazimisha TFF ifanye mabadiliko kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuzingatia viwanja ambavyo klabu za Yanga na Simba zitakuwa zimeamua kuvitumia.
 
Mabadiliko hayo pia yataziathiri timu za African Lyon, Azam, JKT Ruvu, Moro United na Villa Squad ambazo licha ya kutumia Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam, zilipanga mechi zao za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Taifa.
 
Kwa sasa msimamo wa wamiliki wa Uwanja wa Azam ni Yanga na Simba kutoutumia kwa vile uwezo wake wa kuchukua watazamaji ni mdogo.  
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Tuesday, August 16, 2011

Release No. 75 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 16, 2011


MCHEZAJI GERVAIS ANOLD KAGO
Simba imeingia mkataba na mchezaji Gervais Anold Kago kutoka klabu ya Olympic Real de Bangui ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kwa ajili ya kuichezea timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya Vodacom na michuano ya kimataifa.
 
Lakini wakati Kago akiwa bado hajapata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) tumemruhusu achezee timu yake ya Simba kwenye mechi dhidi ya Yanga itakayofanyika kesho (Agosti 17 mwaka huu) kutokana na sababu zifuatazo;
 
Mechi hiyo ni ya Ngao ya Jamii (Community Shield) na lengo lake ni kusaidia jamii. Pili, ni kuzindua msimu mpya wa Ligi na tatu, Simba imeonesha nia ya kumhamisha kutoka CAR.
 
Kwa vile Kago ni mchezaji wa kulipwa ni lazima apate ITC kupitia mfumo wa mtandao wa Transfer Matching System (TMS) ili aweze kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom na michuano ya kimataifa. Hiyo inatokana na ukweli kuwa Simba imeingia mkataba na Kago kama mchezaji wa kulipwa ambaye uhamisho wake ni lazima ufanywe kwa TMS na si ITC ya karatasi ambayo inatumika kwa wachezaji wa ridhaa.
 
Kwa mujibu wa Ibara ya 2(2) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirkisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), mchezaji wa kulipwa ni yule ambaye ana mkataba wa maandishi na klabu na analipwa kutokana na shughuli ya kucheza mpira.
 
Pia si kweli kuwa CAR hawamo kwenye TMS. Nchi hiyo inatumia mfumo huo wa mtandao na Meneja wao wa TMS ni Elie-Delphin Feidangamo.
 
Kwa mujibu wa annexe 3(5) ya Kanuni hizo za FIFA kuhusu uhamisho wa wachezaji, utumiaji wa mfumo wa TMS kwa uhamisho wa wachezaji wa kiume wa kimataifa ni lazima.
 
 
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji

Friday, August 12, 2011

Release No. 73 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 12, 2011


MECHI YA NGAO YA JAMII (COMMUNITY SHIELD)
Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya mabingwa watetezi Yanga na Makamu Bingwa Simba itachezwa usiku (Agosti 17 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa kuanzia saa 2.00 usiku umetokana na sababu kadhaa, kubwa zikiwa mbili; Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na pia Agosti 17 mwaka huu kuwa ni siku ya kazi.
 
Pambano hilo litatanguliwa na mechi ya vikosi vya pili (U20) vya timu hizo ambayo yenyewe itaanza saa 10.30 jioni. Mechi ya Ngao ya Jamii baada ya dakika 90 kama mshindi hatapatikana, zitaongezwa dakika 30. Katika muda huo nao kama mshindi atakuwa bado hajapatikana, itatumika mikwaju ya penalti.
 
Mechi hiyo imepata mwekezaji (Bigbon) na hivi sasa wadau wake wakuu- Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu husika ziko katika mazungumzo ya mwisho mwekezaji huyo. Kwa redio ambazo zinataka kutangaza mechi hiyo moja kwa moja zinatakiwa kuwasiliana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF ili kupewa masharti ya kufanya hivyo.
 
Pia unafanyika utaratibu wa kuuzwa futari uwanjani mara baada ya mechi ya vikosi vya pili ili kuwawezesha washabiki waliofunga kutohangaika kutafuta sehemu ya kufuturu.
 
KAMATI TFF YAMREJESHA MCHAKI
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilikutana Agosti 10 na 11 mwaka huu kujadili rufani ya Frank Mchaki kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kumuengua kugombea nafasi ya Katibu Mkuu katika uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA).
 
Chini ya Mwenyekiti wake Deogratias Lyatto, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa pingamizi lililowekwa dhidi ya Mchaki na kujadiliwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, liliwasilishwa, kujadiliwa na kutolewa uamuzi kinyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 11(2) na (3) kwa kutotanguliwa na pingamizi mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya KIFA, hivyo rufani hiyo haikuwa na sifa ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo baada ya kupitia kiini cha pingamizi, Kamati imefikia uamuzi kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya mrufani zimekosa ithibati.
 
Kutokana na maelezo hayo, Kamati imekubaliana na rufani ya mrufani (Mchaki) dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, hivyo imemrejesha kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa KIFA.
 
Kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 8(3) Kamati ya Uchaguzi ya TFF inauahirisha uchaguzi wa KIFA uliokuwa ufanyike kesho (Agosti 13 mwaka huu) na sasa utafanyika Agosti 20 mwaka huu.
 
USAJILI LIGI DARAJA LA KWANZA
Usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu huu utafanyika baada ya kumalizika Ligi ya Taifa hatua ya fainali inayoendelea hivi sasa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
 
Baada ya fainali hizo kumalizika Agosti 14 mwaka huu TFF itatoa mwelekeo wa usajili huo (roadmap) ikiwemo tarehe ya kuanza na kumalizika, pamoja na kipindi cha pingamizi. Timu tano kutoka kwenye fainali ya Ligi ya Taifa inayoshirikisha timu 12 zitapanda kuingia daraja la kwanza.
 
Ligi Daraja la Kwanza ambayo itaanza katika hatua ya makundi na baadaye kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itashirikisha jumla ya timu 18, na inatarajia kuanza Septemba 3 mwaka huu.
 
Boniface Wambura 
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Monday, August 8, 2011

Release No. 72: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 8, 2011


MECHI YA STARS, SUDAN YAFUTWA
Chama cha Mpira wa Miguu Sudan (SFA) kimefuta mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na timu ya Taifa ya nchi hiyo ‘Nile Crododile’ iliyokuwa ichezwe Agosti 10 mwaka huu.
 
Uamuzi huo umetokana na wakala wa mechi hiyo Hadi Sharkawy kushindwa kupata kwa wakati tiketi ya kuisafirsha Taifa Stars kwenda Khartoum. Pia kutokana na mechi hiyo kufutwa, kambi ya Stars iliyokuwa hapa Dar es Salaam nayo imevunjwa leo.
 
LYON YAPEWA HADI AGOSTI 17 KULIPA WACHEZAJI
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokutana Agosti 7 mwaka huu kupitia masuala mbalimbali imeiagiza klabu ya African Lyon iwe imewalipa wachezaji wake wawili kufikia Agosti 17 mwaka kwa kuvunja mikataba yao na klabu hiyo. Wachezaji ambao kila mmoja anadai sh. milioni 4.3 ni Godfrey Komba na Abdul Masenga.
 
Awali kamati hiyo katika kikao chake cha Januari 7 mwaka huu iliagiza klabu hiyo kutosajili mchezaji mpya msimu wa 2011/2012 hadi itakapokuwa imemaliza suala la wachezaji hao.  Lyon imeomba kusajili wachezaji wapya wanane kati ya 23 inayotaka kuwatumia kwa msimu mpya.
 
Kwa kuzuiwa kusajili wachezaji wapya iwapo haitakuwa imemalizana na Komba na Masenga kufikia Agosti 17, Lyon itakuwa imebaki na wachezaji 15 hivyo kikanuni kutokuwa na sifa ya kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom. Kanuni inaagiza timu inayoshiriki ligi hiyo kuwa na wachezaji wasiopungua 18 na kuzidi 30.
 
PINGAMIZI LA YANGA DHIDI YA SIMBA
Kamati haikusikiliza pingamizi la Yanga dhidi ya Simba kuhusu wachezaji iliyotoa kwa mkopo baada ya kubaini kuwa wachezaji ambao Simba imewatoa kwa mkopo ni wane tu; Haruna Shamte (Villa Squad), Aziz Gilla (Coastal Union), Ahmed Shiboli (Kagera Sugar) na Mohamed Kijuso (Villa Squad).
 
Wachezaji wengine waliotajwa na Simba kupelekwa kwa mkopo katika klabu mbalimbali ilibainika kuwa ni wa kikosi cha pili (U20) ambao hawahusiki na kanuni ya mkopo. Wachezaji wanaoweza kutolewa kwa mkopo ni wa kulipwa tu (wenye mikataba).
 
Kwa upande wa Athuman Idd na Juma Jabu ambao hawakuonekana kwenye orodha ya usajili ya Simba, kamati imesema ni wachezaji halali wa klabu hiyo kwa vile wana mikataba nayo. Idd ana mkataba wa miaka miwili wakati Jabu mkataba wake umebakiza mwaka mmoja kumalizika. Kamati imesisitiza kuwa kitu kikubwa kinachoangaliwa kwenye usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ni mikataba na si kusaini fomu za usajili.
 
MCHEZAJI AMANI PETER KYATA
Kyata aliombewa usajili katika klabu mbili za African Lyon na Yanga. Lyon walimuombea kwa timu ya wakubwa, wakati Yanga walimuorodhesha katika timu ya pili (U20).
 
Kamati ilibaini kuwa mchezaji huyo ni wa kituo cha Tanzania Soccer Academy (TSA) kinachomilikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na hakuna mchakato wowote uliofanyika kumsajili, hivyo usajili wake haujakamilika Yanga wala Lyon.
 
SUALA LA MCHEZAJI OSCAR JOSHUA
Sekretarieti ya TFF imeelekezwa kupeleka suala la mchezaji huyo Polisi kwa ajili ya uchunguzi kwa vile kuna barua mbili zinazopingana kutoka timu yake ya Ruvu Shooting- ya kwanza ikiridhia achezee Yanga na ya pili ikipinga kuwa taratibu hazikufuatwa katika kujiunga na timu yake mpya.
 
Uamuzi huo wa kamati umelenga kubaini ipi ni barua halali kati ya mbili zilizowasilishwa TFF kuhusu usajili wake Yanga, na zote zikionesha kutoka katika timu yake ya Ruvu Shooting.
 
Pia kamati imeamua kuwa kwa vile TFF ilifanyia kazi barua ya kwanza ya kumruhusu kwenda Yanga, hivyo kumpatia leseni, mchezaji ataendelea kutumia leseni hiyo hadi taarifa ya uchunguzi wa Polisi kuhusiana na barua hizo mbili itakapotolewa.
 
HARUNA MOSHI v POULSEN
Kuhusu mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ kutoitikia mwito wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen kucheza mechi kati ya U23 na Shelisheli zilizofanyika Arusha, kamati kwa sasa imeliacha suala hilo kwa kocha huyo kwa vile kuna maagizo ametoa kwa mchezaji huyo.
 
Poulsen amemtaka Boban binfasi kwenda kumueleza sababu ya kutoitikia mwito wake wa kucheza mechi dhidi ya Shelisheli kabla hajafanya uamuzi mwingine kuhusu mchezaji huyo.
 
 
Boniface Wambura 
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Friday, August 5, 2011

TAAFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KOZI YA MAKAMISHNA WA MPIRA WA MIGUU
Kozi ya makamishna wapya kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Taifa na Kombe la Taifa itafanyika ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Agosti 6-8 mwaka huu.

Kwa wanaotaka kuwa makamishna ni lazima washiriki katika kozi ambapo ada ni sh. 10,000. Washiriki wanatakiwa kuwa waamuzi wastaafu na viongozi (administrators) wa mpira wa miguu katika ngazi mbalimbali. Pia wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao halisi (original) vya elimu.

Kutakuwa na mitihani ya kuandika ya sheria za mpira wa miguu na picha (video clips) ambapo watakaofaulu watapata vyeti.

Kwa upande wa makamishna waliopo sasa wa Ligi Kuu, wao watahudhuria kozi hiyo kwa siku moja (Agosti 8 mwaka huu). Kozi itaanza saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni. Washiriki wote wanatakiwa kujitegemea kwa usafiri, chakula na malazi kwa muda wote wa kozi hiyo.

Wakufunzi wa kozi hiyo watakuwa Kapteni mstaafu Stanley Lugenge, Joseph Mapunda na Leslie Liunda.

FAINALI LIGI YA TAIFA
Ligi ya Taifa hatua ya fainali inaanza kesho (Agosti 6 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ikishirikisha timu 12 zilizogawanywa katika makundi matatu ya timu nne. Timu ya kwanza kutoka kila kundi na washindwa bora wawili (best losers)- watafanya jumla ya timu tano zitakazopanda Daraja la Kwanza.

Kundi A lina timu za Polisi Morani (Arusha), Mgambo Shooting (Tanga), Samaria (Singida) na Kasulu United (Kigoma). Polisi Dar es Salaam(Ilala), Majengo (Dodoma), Sifapolitan (Temeke) na Small Kids (Rukwa) ziko kundi B wakati kundi C lina timu za Mlale JKT (Ruvuma), Geita Veterans (Mwanza), Shinyanga United (Shinyanga) na Cosmopolitan (Ilala).
Kila siku zitachezwa mechi mbili ambapo katika ufunguzi kesho mchana Samaria itaumana na Kasulu United wakati jioni ni Polisi Morani na Mgambo Shooting.

Agosti 7 mwaka huu ni Sifapolitan na Small Kids wakati mchezo wa jioni utawakutanisha Polisi Dar es Salaam na Majengo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Thursday, August 4, 2011

Release No. 69: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Agosti 4, 2011


RUFANI YA SHINYANGA UNITED
Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wake Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Mstaafu Alfred Tibagana imekutana leo kusikiliza mashauri mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake.
 
Shinyanga United ilikata rufani kupinga kuenguliwa kwenye fainali hizo, uamuzi uliofanywa na Kamati ya Mashindano ya TFF baada ya klabu hiyo baada ya kutozingatia maelekezo ya TFF kuhusu usajili wa wachezaji wake.
 
Klabu hiyo ilipinga kuenguliwa ikieleza kuwa haikupata taarifa yoyote ya maandishi kutoka TFF ikiwazuia kuwatumia wachezaji ambao usajili wao ulikuwa na matatizo, na pia usajili wao ulifanywa na TFF.
 
Kwa uamuzi huo, Shinyanga United ambayo ilishika nafasi ya tatu katika Kituo cha Kigoma sasa itashiriki katika Fainali za Ligi ya Taifa zinazoanza keshokutwa (Agosti 6 mwaka huu) jijini Tanga.
 
Awali nafasi ya Shinyanga United ilikuwa imepewa timu ya Rumanyika SC ya Mkoa wa Kagera ambayo ilikuwa imeshika nafasi ya nne katika kituo hicho kilichokuwa na timu tano.
 
Boniface Wambura
Media Officer
Tanzania Football Federation (TFF)
Member, CECAFA Media Committee
+255 71 3210242
+255 76 7310242
email: wamburasir@yahoo.com

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation