Friday, March 4, 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Simba Sports Club
Young Africans Football Club

PAMBANO LA YANGA FC v/s SIMBA FC

Tiketi kwa ajili ya mechi namba 108 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya wenyeji Yanga na Simba zimeanza kuuzwa leo asubuhi kama ilivyopangwa. Tiketi hizo zinauzwa katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Big Bon Msimbazi (Kariakoo), Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio na Uwanja wa Uhuru.

Pia tiketi zitaendelea kuuzwa kesho ambayo ni siku ya mchezo katika maeneo hayo kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 6 mchana. Baada ya muda huo zitaendelea kuuzwa Uwanja wa Uhuru pekee.

Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili na TFF inasisitiza kuwa watu wote wanatakiwa kuingia uwanjani kwa kutumia tiketi. Kwa maana hiyo hakutakuwa na pasi maalum (free pass).

HAKI ZA TELEVISHENI

Tunapenda kukumbusha kuwa haki ya kuonesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom iko kwa kampuni ya Sahara Media Group kupitia kituo chake cha televisheni cha Star. Hivyo vituo vingine vya televisheni vinaruhusiwa viwanjani kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom kwa ajili ya kuchukua picha za habari tu na si kurekodi mechi nzima.

Televisheni nyingine zinaweza kurekodi mechi nzima kwa makubaliano na Sahara Media Group ambayo ndiyo yenye haki hizo.

FAINALI ZA U20 LIBYA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) bado linafuatilia machafuko ya kisiasa nchini Libya kabla ya kufanya uamuzi wa mahali na tarehe ambayo fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitafanyika.

Fainali hizo zilipangwa kufanyika kuanzia Machi 18 hadi Aprili Mosi mwaka huu jijini Tripoli, Libya. Mara baada ya kufanya uamuzi, CAF itatuma taarifa mara moja kwa wanachama wake.

Mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ni miongoni mwa waamuzi walioteuliwa na CAF kuchezesha fainali hizo.

Boniface Wambura

Ofisa Habari

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation