Tuesday, May 3, 2011

TAARIFA MUHIMI MBALIMBALI

TAIFA STARS v BAFANA BAFANA


Timu ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ inatarajia kuwasili nchini Mei 12
mwaka huu kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania
‘Taifa Stars’ itakayofanyika Mei 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.


Nyota wote wa kikosi cha kwanza cha Bafana Bafana kinachofundishwa na Pitso
Mosimane wanatarajiwa kuwepo kwenye mechi hiyo, isipokuwa kiungo Steven Pienaar
anayechezea timu ya Tottenham Hotspurs inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza.

Bafana Bafana na Stars zote zina mechi ngumu ugenini za mchujo kusaka tiketi za
fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) zitakazofanyika mwakani Equatorial
Guinea na Gabon. Stars itacheza Juni 4 mwaka huu jijini Bangui dhidi ya Jamhuri
ya Afrika ya Kati wakati Bafana Bafana itakuwa jijini Cairo, Juni 3 dhidi ya
wenyeji Misri.

Stars itaingia kambini Mei 7 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo. Wachezaji
Idrissa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya, Henry Joseph (Kongsvinger IL,
Norway), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam),
Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) na Athuman Machupa (Vasalund IF,
Sweden) wameshaombewa ruhusa katika klabu zao ili wajiunge na Stars kwa ajili ya
mechi hiyo.


MAPATO U23 TANZANIA v UGANDA (THE KOBS)
Pambano la mchujo la All Africa Games kati ya Tanzania U23 na Uganda U23 (The
Kobs) lililochezwa Aprili 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza
sh. 32,982,000 kutokana na watazamaji 24,078 walionunua tiketi.Watazamaji 22,117
walilipa sh. 1,000, 1,749 (sh. 5,000) na 212 (sh. 10,000).

Baada ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 5,031,152.54 na gharama
za awali za mchezo sh. 16,950,000 mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; uwanja sh.
1,100,084.75, gharama za mchezo sh. 1,100,084.75, Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) sh. 550,042.37 wakati TFF sh. 8,250,635.59. Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata asilimia tano ya mgawo wa TFF ambayo
ni sh. 412,531.78.

Boniface Wambura
Ofisa Habari TFF
Ref:
TFF/ADM/EC.11/----
03 Mei 2011

Mwenyekiti
Kamati ya Uchaguzi
Villa Squad Football Club
DAR ES SALAAM


YAH: UCHAGUZI WA VIONGOZI WA VILLA SQUAD FOOTBALL CLUB

Rejea barua ya TFF yenye Kumbukumbu Na. TFF/ADM/EC.11/09 ya tarehe 30 Aprili
2011 kuhusu somo hilo hapo juu iliyotimwa kwa Katibu wa Villa Squad Football
Club.

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inaaiagiza
Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Villa Squad kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za
wanachama wa TFF katika mchakato wa uchaguzi uliotajwa hapo juu.


Ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi, Kamati
ya Uchaguzi ya Villa Squad inakumbushwa kuzingatia viwango vya ada ya fomu za
kuomba uongozi na pia tunaambatanisha ratiba ya mfano inayokidhi matakwa ya
Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF kwa urahisi wa rejea na kwa utekelezaji
wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Villa Squad.

Wako katika michezo,

Angetile Osiah
KATIBU MKUU

RATIBA YA UCHAGUZI WA VILLA SQUAD FOOTBALL CLUB



Na. TAREHE SHUGHULI
1. 02/05/2011 Kamati ya Uchaguzi ya VILLA SQUAD FOOTBALL CLUB (VILLA) kutangaza
Uchaguzi wa VILLA na nafasi za kugombea.


2.
03/05/2011 – 08/05/2011
Kuchukua fomu za kugombea uongozi VILLA. Mwisho wa kurudisha fomu ni tarehe
08/11/2011 saa 10:00 Alasiri.


3.
10/05/2011
Kamati ya Uchaguzi kupitia fomu za waombaji uongozi VILLA.

4.
11/05/2011
Kutangaza matokeo ya upitiaji fomu na kuweka wazi kwenye mbao za matangazo
majina ya waombaji uongozi VILLA.

5. 12/05/2011- 16/05/2011 Kutoa fursa ya pingamizi (kama zipo) kwa waombaji
Uongozi. Mwisho wa kupokea pingamizi ni tarehe 16/05/2011 saa 10:00 Alasiri

6. 18-20/05/2011 Usaili na kutangaza matokeo /Kuwajulisha wagombea matokeo ya
usaili.

7. 21 – 22/05/2011 Kutoa fursa ya kukata Rufaa, kwenye Kamati ya Uchaguzi ya
TFF. Mwisho wa kupokea Rufaa ni tarehe 22/05/2011 saa 10:00 Alasiri.


8.
23-27/05/2011
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kusikiliza rufaa (kama zipo) na kutangaza matokeo ya
rufaa. (Kama hakuna rufaa, Kamati ya uchaguzi ya VILLA kutangaza majina ya
wagombea na nafasi zao na kuanza kwa Kampeni.)


10.
28/05/2011
Baada ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Uchaguzi ya VILLA
kutangaza majina ya wagombea na nafasi zao na kuanza Kampeni.


11.
05/06/2011
Uchaguzi wa Viongozi wa VILLA SQUAD.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation