Tuesday, March 8, 2011

Tenga ashukuru wadau kwa uteuzi

Leodegar Chilla Tenga

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chilla Tenga amewashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono na wote waliofanikisha yeye kushinda Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Caf.

Tenga alichaguliwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kumshinda Celestine Musabiyima wa Rwanda aliyekuwa akitetea nafasi hiyo uchaguzi uliofanyika Khartoum, Sudan.


Tenga, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), amesema atatumia wadhifa huo kusaidia maendeleo ya soka kwa ukanda huu.


Pia amesema atashirikiana na viongozi wa kanda nyingine kuhakikisha kuwa soka la Afrika Mashariki linapiga hatua.


Aliishukuru TFF kwa kumdhamini agombee nafasi hiyo na kumuunga mkono na kuwashukuru Watanzania kwa kumfanikisha afikie hatua hiyo.


Alieleza changamoto mbalimbali ambazo zinamkabili, lakini aliahidi kwa kadri ya uwezo wake atahakikisha anapambana nazo na soka la Afrika Mashariki na Kati linasonga mbele.


Tenga, ambaye pia huitwa kwa jina la 'Sir' kwa kuthaminiwa mchango wake katika soka ndani na nje ya nchi, anakuwa Mtanzania wa pili kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya Caf baada ya Said Hamad El Maamry ambaye aliwahi kushinda nafasi hiyo mwanzoni mwa miaka ya 80 kwa vipindi viwili mfululizo.


Alishindwa kutetea nafasi hiyo katika kipindi cha tatu baada ya TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu (FAT) kutoidhinisha jina lake Caf.


El Maamry hivi sasa ni mjumbe wa heshima wa CAF.


Mtanzania mwingine aliyewahi kuwania nafasi hiyo mara mbili, lakini hakufanikiwa kushinda ni Muhidin Ndolanga ambaye aliwania wakati huo akiwa Mwenyekiti wa FAT.

Chanzo: Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation