

TIMU ya nyota wa zamani ‘All Stars’ waliowahi kukipiga katika klabu ya Simba, jana waliibuka kidedea katika mechi maalumu ya kuwachangia waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto baada ya kuwalaza mahasimu wao Yanga kwa bao 1-0.
Katika mechi hiyo iliyovuta hisia za mashabiki wengi wa soka kutaka kuona vitu adimu vya nyota hao wa zamani, pande zote zilianza mchezo kwa kasi ili kutaka kujipatia bao la mapema.
Walikuwa ni Simba waliofanya shambulizi katika dakika ya 6 tu ya mchezo, lakini shuti la Yussuf Macho ‘Musso’ lilidakwa na kipa Peter Manyika, huku Edwin Mukenya katika dakika ya 14, akifanya kazi ya ziada ya kuwapangua wachezaji wa Yanga lakini alishindwa kumalizia kuukwamisha wavuni mpira.
Dakika ya 15 Yanga walijibu mashambulizi lakini Ally Yussuf aliyeukwamisha mpira wavuni alikuwa ameotea.
Simba walijipatia bao la kwanza dakika ya 34 kwa mkwaju wa adhabu wa Shekhan Rashid uliokwenda moja kwa moja nyuzi 90, baada ya Ally Mayai kumwangusha Yussuf Macho nje ya 18. Bao lililodumu hadi dakika 45 za kwanza.
Kipindi cha pili, licha ya mabadiliko kwa timu zote na Yanga kujaribu kuchomoa bao lao kupitia kwa washambuliaji wake Ben Mwalala na Edibily Lunyamila, lakini ngome ya Simba ilikuwa makini kuondosha hatari zote, hivyo hadi filimbi ya mwisho, Simba 1, Yanga 0.
Simba: Issa Manofu, Abubakar Kombo/ Bakari Idd/ Tom Kipese ‘Uncle Tom’, Ramazani Wasso, Said Kokoo, Boniface Pawasa, Edwin Mukenya, Said Sued, Shekhan Rashid, Madaraka Selemani ‘Mzee wa Kiminyio’/ Kamba Lufo, Bita John/ Haruna Moshi ‘Boban na Yussuf Macho ‘Musso’/ Mrisho Moshi.
Kocha: Madaraka Selemani.
Yanga: Peter Manyika, Omar Kapilima, Mwanamtwa Kihwelo/ Chibe Chibindu, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Shabani Ramadhani, Waziri Mahadhi/Idd Moshi, Steven Nyenge/ Deo Lucas, Sekilojo Chambua/ Oscar Makoye, Salvatory Edward ‘Doctor’/ Akida Makunda, Ally Yussuf ‘Tigana’/ Ally Mayai ‘Tembele’, Ben Mwalala/ Kudra Omar na Edibily Lunyamila/ Omar Changa.
Kocha: Ken Mwaisabula ‘Mzazi’.
0 comments:
Post a Comment