Tuesday, March 8, 2011

Maombi ya Simba kusogeza mbele mchezo wao na Ruvu Shooting Stars yakataliwa

Kikosi cha Simba SC

Ombi la klabu ya Simba kutaka mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting Stars uliopangwa kuchezwa leo mjini Morogoro usogezwe mbele limekataliwa na TFF wa kuhofia upangaji wa matokeo.

Awali, Simba iliwasilisha barua T FF ikiomba mchezo huo ambao awali ulipangwa kufanyika Januari 15 mwaka huu usogezwe mbele na kufanyiwa hivyo hadi Machi 9 kutokana na timu hiyo kuwa na mchezo wa kimataifa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Elan ya Comoro.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala aliiambia Mwananchi jana kuwa waliomba kusogezewa mbele tena mchezo huu ili timu yao iweze kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kukutana na mabingwa wa Afrika na namba mbili wa dunia, TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utakaochezwa Machi 20 mjini Lubumbashi.

Alisema hata hivyo mpaka jana walikuwa hawajajiwa na TFF, hivyo wameamua kuondoka jana mchana kwenda Morogoro ili kuwahi mchezo wao huo wa kesho.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah aliiambia Mwananchi jana kuwa wamekwishawajibu Simba kuwa kwa sasa hawawezi kupangua ratiba kwa vyovyote vile kwa ajili ya kuhofia upangaji wa matokeo katika michezo ya mwisho mwisho.

''Tumekwishawaambia Simba kuwa hatutapangua ratiba yetu tena tunahofia upangaji wa matokeo kwa baadhi ya timu, kwa hiyo mchezo huu utaendelea kesho kama kawaida kwa kuwa barua yao imesema kuwa wanataka kujiandaa na mchezo wa TP Mazembe kwa kuweka kambi mjini Arusha kwa kuwa hali ya hewa ya Arusha ni sawa na Congo, tunaamini mchezo wa ligi ni sehemu ya maandalizi hayo, '' alisema Osiah.

Alisema ratiba hiyo ya kambi haikuwepo katika upangaji wa ratiba ya awali, hivyo imekuja hivi karibuni na wao hawahusiani na lolote kuhusu hilo na mechi zao zitakuwa kama zilivyopangwa awali.

Baada ya mchezo huo wa kesho, Simba pia itakuwa na mchezo mwingine Jumamosi dhidi ya AFC ya Arusha, mahali ambako ndiko wataweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Mazembe badala ya Nairobi, Kenya kama walivyotangaza awali.

Wakati huo huo, Jessca Nangawe anaripoti kuwa Ligi Kuu ya Vodacom itaendelea leo kwenye Uwanja wa Uhuru , Dar es Salaam ambapo African Lyon watakuwa wenyeji wa Polisi Tanzania.

Lyon inaingia uwanjani ikiwa na lengo la kushinda mchezo huo ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri katika ligi hiyo huku Polisi nao wakisaka ushindi ili kujiondoa katika nafasi ya kushuka daraja.

Katika msimamo wa ligi, Lyon iko mbele ya Polisi Dodoma kwa pointi mbili ikiwa nazo 19 dhidi ya 17 za maafande hao.

Chanzo: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
The Official Blog of Tanzania Football Federation