TIMU ya Villa Squad ya Dar es Salaam jana imefanikiwa kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya kutoka 0-0 na Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Mchezo huo wa fainali za ligi daraja la kwanza hatua ya tisa bora ulikuwa na ushindani mkubwa na mashabiki walishuhudia dakika 90 zikimalizika bila miamba hiyo kufungana.
Matokeo hayo yameifanya Villa Squad iliyoshuka daraja msimu wa mwaka 2008/2009 ifikishe pointi 12 sawa na Polisi Morogoro ambayo jana iliifunga JKT Oljoro bao 1-0, lakini Villa ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kulingana na msimamo wa ligi hiyo, Villa ina pointi 12 mabao 12 ya kufunga, matano ya kufungwa, wakati Polisi ina pointi 12 mabao manane ya kufunga na manne ya kufungwa.
Kwa mazingira hayo, Villa sasa inaungana na JKT Oljoro inayoongoza ligi ikiwa na pointi 15, Coastal Union inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 13 kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2010/2011.
Timu ya nne itategemea matokeo ya mchezo wa leo kati ya Moro United inayoshika nafasi ya sita ikiwa na pointi kumi na Morani inayoshika mkia ikiwa na pointi mbili, ambao utafanyika alasiri kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Kama Moro United itashinda mchezo huo itafikisha pointi 13, hivyo itakuwa imepanda daraja kwa kushika nafasi ya pili ama ya tatu kutegemeana na uwiano wake wa pointi na Coastal Union, lakini kama itafungwa ama kutoka sare basi Polisi Morogoro yenye pointi 12 ambayo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi itakuwa ndiyo imepanda daraja.
Rhino ya Tabora inayoshika nafasi ya tano ikiwa na pointi 11 haina matumaini ya kupanda daraja kutokana na matokeo ya mechi za Februari 20.
Timu nne za juu ndizo zinapanda daraja katika ligi hiyo inayoshirikisha timu tisa.
Prisons ya Mbeya inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi tisa, wakati TMK United inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi sita na leo inamaliza ligi kwa kucheza na Coastal alasiri.
0 comments:
Post a Comment